LONDON, England
Kiungo wa kati wa Arsenal, Declan Rice, amesema timu yake iko kwenye nafasi nzuri ya kuwawinda Liverpool katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.

Hii ni baada ya Arsenal kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Manchester City juzi, Jumapili. Rice alitoa pasi mbili za mabao, huku akisisitiza kuwa The Gunners hawapo tayari kuachana na mbio za ubingwa.
Liverpool kwa sasa wanaongoza ligi wakiwa na pointi sita zaidi ya Arsenal, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Licha ya Liverpool kuonekana kuwa na kasi nzuri kuelekea kutwaa taji lao la 20, Rice anaamini bado kuna nafasi ya kuwapindua.
“Liverpool bado wako mbali mbele, hasa wakiwa na mchezo mkononi, lakini lazima tushinde kila mchezo uliopo mbele yetu,” Rice aliambia Sky Sports.
“Tumepoteza pointi muhimu, kama dhidi ya Aston Villa tulipokuwa mbele kwa mabao 2-0 lakini tukaruhusu sare. Kama tungekuwa na alama hizo, tungekuwa karibu zaidi na Liverpool.
“Lakini bado tupo kwenye mbio, tutaendelea kusukuma. Tunahitaji wengine wa kutusaidia, lakini tunajua lengo letu ni kuwawinda na kutwaa ubingwa msimu huu,” aliongeza Rice.
Katika ushindi wao dhidi ya City, mabao ya Martin Ødegaard, Thomas Partey, Myles Lewis-Skelly, Kai Havertz, na Ethan Nwaneri yaliifanya Arsenal kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alisema amefurahishwa na namna timu yake ilivyocheza, akimtaja kijana Myles Lewis-Skelly kuwa mchezaji wa kuangaliwa baada ya kufunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo.
“Tulihitaji ushindi huu, na namna tulivyoupata imenifurahisha sana,” alisema Arteta. “Tulifunga mabao mazuri na timu ilionesha kiwango bora cha ushindani.”