Saturday, December 6, 2025
spot_img
HomeHabariSalome Makamba aipa kongole PBPA kuimarisha akiba ya mafuta nchini

Salome Makamba aipa kongole PBPA kuimarisha akiba ya mafuta nchini

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, ameipongeza Wakala ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa utendaji kazi mzuri na hatua madhubuti inazochukua kuhakikisha Tanzania inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha muda wote.

Akizungumza na Menejimenti ya PBPA leo Desemba 6, 2025 jijini Dar es Salaam, Makamba amesema wakala huo umeonyesha ufanisi mkubwa katika kusimamia mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja, jambo ambalo limeisaidia nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, lakini hakikisheni mnatoa elimu kwa Watanzania kuhusu majukumu na kazi zenu,” amesema Makamba.

Vilevile, ameitaka PBPA kuongeza ushirikiano na kuwawezesha Watanzania wazawa kuingia katika biashara ya mafuta, akisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa ndani katika sekta hiyo.

“Lazima tupate wawekezaji wa Tanzania. Tuwawezeshe waingie kwenye hii biashara,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, amesema wakala umefanikiwa kudhibiti upatikanaji wa mafuta kwa kuhakikisha kuna akiba ya kutosha, kuwepo kwa takwimu sahihi za bidhaa hiyo pamoja na kuiwezesha Serikali kupanga mapato kwa ufanisi.

“Mfumo wa Bulk Procurement System (BPS) umesaidia hata nchi za jirani kuagiza mafuta kwa zaidi ya asilimia 95, sambamba na kudhibiti ubora wa mafuta yanayoingia nchini,” amesema Simon.

Ameongeza kuwa nchi kama Malawi, Zambia, Uganda, Rwanda, Zimbabwe na Namibia zimekuwa zikitembelea Tanzania mara kwa mara ili kujifunza namna bora ya kusimamia uagizaji mafuta kupitia mfumo wa BPS.

Simon amesema PBPA imefanikiwa kuratibu uagizaji mafuta kwa ufanisi kutokana na uwazi uliopo kwenye mchakato mzima wa uagizaji, hatua ambayo imejenga imani ndani na nje ya nchi.

Ziara ya Makamba katika ofisi za PBPA imelenga kujifunza kwa kina kuhusu majukumu ya wakala huo pamoja na kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Waziri wa Nishati.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments