Michezo miwili ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa juzi Jumapili katika Uwanja wa Cairo, Kiwengwa, Kisiwani Unguja, ilimalizika kwa sare.

Vinara wa ligi hiyo, Mlandege FC, walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Maafande wa Zimamoto SC katika mchezo uliopigwa majira ya saa nane mchana.
Katika mchezo mwingine uliochezwa saa 10 alasiri, majirani wa Mwembe Makumbi City na JKU SC nao walimaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kocha Mkuu wa Mlandege FC, Hassan Ramadhan, alisema matokeo hayo hayakuwa wanayotarajia, lakini alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu.
“Mchezo ulikuwa na upinzani mkali kwa dakika zote 90. Tulitanguliwa kufungwa lakini wachezaji wangu hawakukata tamaa, wakaendelea kupambana hadi wakasawazisha,” alisema Ramadhan.
Kocha huyo aliongeza kuwa sasa wanajipanga kwa mchezo wao unaofuata dhidi ya Chipukizi FC kisiwani Pemba.
Katika mchezo mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Finya, Pemba, Junguni United walifanikiwa kujinasua kutoka katika mstari wa kushuka daraja baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Chipukizi FC.
Ligi Kuu Zanzibar mzunguko wa 17 itaendelea Alhamisi kwa michezo miwili, ambapo Inter Zanzibar FC watachuana na JKU SC, huku Junguni FC wakiwakaribisha Uhamiaji FC.