Aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu za Simba SC na Yanga SC, Senzo Mbatha, ameteuliwa rasmi kuwa CEO mpya wa TRA United FC.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, Senzo amepatiwa jukumu la kuandaa na kusimamia masuala yote ya utawala na uendeshaji wa timu, sambamba na kuimarisha mifumo ya kiutendaji kulingana na mwelekeo mpya wa klabu.
Uongozi wa TRA United FC umesema unatarajia uzoefu mkubwa wa Senzo katika uongozi wa soka barani Afrika utakuwa chachu ya maendeleo ya klabu hiyo, hasa katika kuboresha miundombinu ya usimamizi, nidhamu ya kiutawala, na mikakati ya kibiashara ndani ya timu.
Senzo Mbatha, ambaye pia aliwahi kufanya kazi kwenye Orlando Pirates FC ya Afrika Kusini, amekuwa miongoni mwa viongozi wenye rekodi nzuri katika uendeshaji wa vilabu vikubwa vya soka Afrika Mashariki.
Ujio wake ndani ya TRA United FC unatarajiwa kuleta sura mpya katika usimamizi wa timu hiyo na kuinua hadhi yake kwenye mashindano ya ndani na nje ya nchi.




