Wednesday, December 10, 2025
spot_img
HomeHabariSerikali yasitisha shughuli za kibinadamu Mto Ruvu

Serikali yasitisha shughuli za kibinadamu Mto Ruvu

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) kuhakikisha kiwango cha maji kinachopatikana kwa sasa kinagawiwa kwa usawa ili maeneo yote yafaidike na huduma hiyo.

Aweso alitoa maelekezo hayo leo, Desemba 10, alipotembelea chanzo cha maji cha Mtambo wa Ruvu Juu, Mlandizi, Wilaya ya Kibaha, kwa ajili ya kukagua hali ya upatikanaji wa maji katika kipindi ambacho mvua hazijaanza kunyesha maeneo kadhaa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Aweso amesema ni muhimu maji yaliyopo yagawiwe kwa uadilifu, huku akisisitiza kuwa kipaumbele kipo kwenye matumizi ya nyumbani wakati oparesheni za usimamizi na ufuatiliaji zikiendelea.

Aidha, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutunza na kuhifadhi maji, hasa katika kipindi hiki cha upungufu wa mvua na kupungua kwa mtiririko wa maji kwenye vyanzo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bonde la Wami–Ruvu, Elibariki Mmasi, amesema baada ya kubaini changamoto ya upatikanaji wa maji katika mtambo huo, mamlaka ilianzisha oparesheni maalumu ya kusitisha shughuli za kibinadamu katika Mto Ruvu.

Mmasi ameeleza kuwa oparesheni hiyo imeleta matokeo chanya, ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha maji katika mto huo, hatua iliyowezesha mtambo wa Ruvu Juu kuendelea kuzalisha maji kwa mahitaji ya wananchi.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kusitishwa kwa shughuli za kibinadamu katika Mto Ruvu kutaendelea hadi pale hali ya maji itaonyesha kuimarika, kutegemea mwenendo wa mvua katika maeneo mbalimbali.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments