Serikali mkoani Morogoro inatarajia kutumia huduma za Treni ya mwendo kasi (SGR) kusafirisha mazao ya mbogamboga katika mikoa ya Dodoma, Dar Es salaam na nchi za nje ili kunusuru hasara wanazopata wakulima kwa mazao kuharibika wakati wa uvunaji shambani na kukosa uwezo wa kuyatunza kabla ya kuyafikisha sokoni.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari na wadau wa biashara juu ya Maonesho ya biashara mkoa wa Morogoro (MRTFE) yaliyoandaliwa na Chemba ya wafanyabiashara, wenye viwanda na Kilimo (TCCIA) yanayotarajia kufanyika kuanzia Novemba 20 hadi 30 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
”masoko makuu ya mbogamboga yapo jijini Dodoma na Dar es salaam kwa hapa nchini lakini bidhaa zingine zimekuwa zikisafirishwa hadi nje ya nchi, usafiri wa SGR ni mwepesi na kwa kusafirisha bidhaa hizo kwa kuanza na uhifadhi wa bidhaa hizo kwenye moja ya behewa katika stesheni za kituo cha Morogoro na Kilosa, kwa mtindo wa kuwekwa kwenye jokofu, utasaidia mazao ya wakulima kubaki kuwa bora hadi yatakapofika sokoni kwa wanunuzi” alisema Malima.
Malima anasema mkoa wa Morogoro ni kituo cha mazao mbalimbali ya chakula ikiwemo mbogamboga, viungo na chakula ambapo tayari wameshawekeza kwenye zao la Parachichi na Kakao na kufanya Morogoro kuwa wa pili kwa uzalishaji wa mazao hayo baada ya mikoa mikuu inayozalisha.
Afisa Uendelezaji biashara Mwandamizi kutoka Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Morogoro Grace Makoye amewataka wafanyabiashara wadogo na wa kati kujitokeza kwenye maonesho hayo ili kufahamu teknolojia mbalimbali zitakazooneshwa, kutengeneza ushirikiano na wengine, kujua fursa za mikopo na kutanua wigo kwenye masoko ya bidhaa.
Mwenyejiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro Mwadhini Myanza amesema lengo kuu la maonesho hayo ni kushirikisha wajasiliamali kutanua Mawazo ya kibiashara na baadae kuunda vikundi kutoka sekta mbalimbali na kuendelea kutoa elimu ili kukuza Uchumi wa mmoja na vikundi kwa ujumla.
Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘kukuza ujasiriamali, ubunifu na uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo jumuishi ya kiuchumi na kijamii’ yanatarajia kuzinduliwa Novemba 24 na mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima huku yakiwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo wadau wa kilimo, wananchi, wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, Serikali na wawekezaji.




