Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) mkoa wa Njombe, Sigrada Mligo, amesema ataendelea kuwasemea wananchi wa mkoa wa Njombe ili kupatikana kwa suluhisho la changamoto zinazowakabili, hasa katika maeneo ya miundombinu ya barabara na uwanja wa ndege.

Akizungumza katika hafla ya pongezi iliyoandaliwa na chama hicho mjini Njombe, Sigrada alisema atahakikisha mkoa huo unapata vyuo vya michezo, pamoja na kushughulikia suala la kupunguza bei ya vifaa vya ujenzi ili kuwawezesha wananchi kufanikisha miradi yao.
Aidha, amesisitiza kuwa ataendelea kushinikiza serikali kutekeleza mfumo wa bima ya afya kwa wote, kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili ili ziwezekane kueleweka kwa wananchi, pamoja na kupatikana kwa katiba mpya.





