Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeElimuStanbic yatoa meza, viti na miche ya miti kwa Shule ya Sekondari...

Stanbic yatoa meza, viti na miche ya miti kwa Shule ya Sekondari Ihombwe

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kulinda tunu za taifa — ikiwemo amani, umoja na mshikamano — kuelekea msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025.

Wito huo umetolewa Desemba 4, 2025 katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kupitia Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Jenerali Majid Hassan Sulumbu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye hafla ya kukabidhi meza 120, viti 120 pamoja na miche 100 ya miti vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20. Vifaa hivyo vimetolewa na Benki ya Stanbic kwa ajili ya Shule ya Sekondari Ihombwe iliyopo Kata ya Utengule Usangu, wilayani Mbeya Vijijini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Jenerali Sulumbu, alisema msaada huo wa Benki ya Stanbic ni mchango muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwenye kuboresha mazingira ya elimu. Aliipongeza benki hiyo kwa kujitoa na kuwataka wadau wengine kuendelea kushiriki katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Awali, Meneja wa Benki ya Stanbic, Tawi la Mbeya, Paul Mwambashi, alitoa wito kwa jamii kuendelea kutumia huduma za benki hiyo, akibainisha kuwa kwa zaidi ya miaka 30 imekuwa mstari wa mbele kutoa huduma bora na salama kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ihombwe, Mwalimu Zackia Hassan Mwangu, aliishukuru Benki ya Stanbic kwa msaada huo wa madawati, viti na miche ya miti, akisema umefika wakati muafaka. Alitoa rai kwa Watanzania kuiga mfano huo kwa kuchangia maendeleo ya elimu katika maeneo yao kupitia mahitaji ya ziada na kiada.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments