Tuesday, March 31, 2026
spot_img
HomeGeneral NewsTanzania kuwa kitovu cha viwanda Afrika

Tanzania kuwa kitovu cha viwanda Afrika

Tanzania imeelezwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za madini ya chuma, vanadiamu na titaniamu, ambazo zinatarajiwa kuchimbwa na kusindikwa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri Salum, jijini Dodoma wakati wa kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Fangda Group, Ao Xinhua, pamoja na ujumbe wake.

Kikao hicho kililenga kutathmini fursa za uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji viwandani na uongezaji thamani wa rasilimali barani Afrika.

Balozi Salum alisisitiza kuwa lengo la Serikali si kusafirisha malighafi pekee, bali ni kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za mwisho, hatua itakayosaidia kuongeza ajira kwa wazawa, kukuza ujuzi wa kiteknolojia na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza bidhaa kutoka nje.

Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imejipambanua kama lango la soko lenye zaidi ya watu milioni 300 kupitia jumuiya za East African Community (EAC) na Southern African Development Community (SADC). Alitaja miundombinu ya Standard Gauge Railway (SGR) na Bandari ya Dar es Salaam kuwa chachu ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani zisizo na bandari.

Aliwahimiza wawekezaji hao kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji huku akiahidi kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuweka vivutio vya kodi na kurahisisha taratibu ili kuvutia miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Ao Xinhua alisema Fangda Group ina dhamira ya kujenga uwezo wa uzalishaji ndani ya Afrika, kuongeza thamani ya rasilimali, pamoja na kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga na biashara, ikiwa ni sehemu ya kusaidia mapinduzi ya viwanda na kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi barani humo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments