Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya tenisi kwa walemavu, Riziki Salum, ametangaza kuwa maandalizi ya mashindano ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia yameanza rasmi.

Mashindano hayo ya kufuzu kwa mataifa ya Afrika yatafanyika Februari 2-25 mwakani nchini Morocco.
Salum amesema timu hiyo inalenga kuunda kikosi imara kupitia mashindano ya maandalizi yanayotarajiwa kufanyika Januari 2024, yatakayowezesha kuchagua wachezaji wenye viwango vya juu.
Hata hivyo, kocha huyo ameeleza changamoto ya ukosefu wa rasilimali, akiomba taasisi na makampuni kuunga mkono juhudi za timu hiyo ili kufanikisha ushiriki wao na kuiwakilisha Tanzania kwa heshima.
“Tunawaomba wadau wa michezo watuunge mkono ili tuweze kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano haya muhimu,” alisema Salum.