Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema chama hicho kinatekeleza mambo kwa uhakika siyo ‘tone tone’ hivyo amewaomba Watanzania kukichagua katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Amewasihi Watanzania kuchagua mafiga matatu (wabunge, madiwani na Rais wote wa CCM), ifakapo Oktoba 29, siku ya kupiga kura.
Dk. Samia ameeleza hayo leo Jumapili wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni wilayani Kondoa mkoani Dodoma, katika mwendelezo wa kunadi sera za CCM na kuomba kura kwa Watanzania.
Mgombea huyo, ameingia siku ya pili ya ziara yake mkoani Dodoma, baada ya kuihitimisha katika mkoa wa Morogoro ambapo aliwaeleza wananchi wa mkoa huo mambo yaliyofanyika na yatakayofanyika endapo watampa tena ridhaa ya kuongoza.
“Chagueni mafiga matatu, Serikali haendi na tone tone bali inatoa fedha za maendeleo. Tunapotoa fedha madiwani hawa ndio Bunge lenu, ambapo wanakaa na kuangalia fedha zilizoletwa na miradi iliyopangwa, itekelezwe vipi ili kusimamia,” amesema.
“Najiombea kura mimi, lakini nawaombee madiwani na wabunge ili wakasimamie kazi hiyo. Naomba niletee hawa, watakuja kunadi ilani ya CCM, niwaombe sana Oktoba 29, twende tukakipigie kura Chama Cha Mapinduzi,” ameongeza Dkt Samia.
Dkt Samia amesema CCM, ndiyo chama kinachojali utu na mtu, ndio maana kimekuja na kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’.
Amewaahidi mambo makubwa wananchi wa Chamwino, Chemba na Kondoa endapo watampa tena ridhaa ya kuongoza Serikali.




