Tuesday, December 16, 2025
spot_img
HomeHabariTutafundisha teknolojia inayolinda desturi zetu

Tutafundisha teknolojia inayolinda desturi zetu

Pamoja na dhamira yake ya kukuza uchumi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake pia, itahakikisha inajenga kizazi kijacho chenye maadili kwa maslahi ya Taifa.

Utekelezwaji wa hilo, kwa mujibu wa Dkt Samia, utafanyika kwa kuhakikisha teknolojia itakayofundishwa shuleni na kutumika inalinda mila, desturi na tamaduni za nchi, zipewe hadhi ili vijana wazifuate, badala ya kuiga za nje.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo Mjini Mtwara leo, Ijumaa Septemba 26, 2025, alipozungumza na wananchi wa mkoa huo, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais, zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Akiijenga hoja hiyo, Dkt Samia amesema dhamira yake katika miaka mitano ijayo ni kupiga hatua kubwa za matumizi ya teknolojia wakati huo huo, hatua za makusudi zikichukuliwa kudumisha, mila, desturi na tamaduni.

“Miaka mitano ijayo itakuwa miaka ya kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia za kisasa na vile vile miaka mitano ijayo tunataka kuchukua hatua za makusudi kudumisha mila na desturi zetu zile zilizo bora,” amesema.

Katika kufanikisha hilo, amesema teknolojia itakayofundishwa itaunganishwa na mila, desturi na tamaduni za Tanzania ili isifute, kuharibu, au kuwapotosha vijana wakakiuka mila na desturi.

“Kwa kadri inavyowezekana teknolojia tunayokwenda kuitumia tunataka ikalinde mila, desturi na tamaduni zetu na tuzirithishe kwa vijana wetu badala ya kuona tamaduni za nje na wakazifuata, wafuate hizi za kwetu, tuzipe hadhi wazifuate hizi za kwetu,” amesema.

Dkt Samia amesema malengo yake ni kuhakikisha kinajengwa kizazi zijacho chenye maadili ili kuondoa ombwe la maadili linalolalamikiwa na viongozi wa dini kwa sasa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments