Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kuwafunga makandarasi wa kampuni ya China First Highway Engineering Co. Ltd kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa ujenzi wa barabara mkoani Dodoma, licha ya Serikali kulipa sehemu ya malipo kwa wakati.
Waziri Ulega amesema juhudi za kuwahamasisha vigogo wa kampuni hiyo kuja nchini na kutoa maelezo kuhusu ucheleweshaji wa kazi zimegonga mwamba. Amesema sasa kuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani kwa ukiukaji wa mkataba, huku akisisitiza kuwa makandarasi wanaotimiza majukumu yao wataenziwa, lakini wale wanaoshindwa watachukuliwa hatua kali.
Ulega ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumshikilia na kumuhoji mkandarasi aliyeshindwa kufikisha asilimia 13 ya utekelezaji wa mradi huo. Aidha, ameagiza Naibu Katibu Mkuu, Dk Charles Msonde, kufuatilia miradi mingine ya mkandarasi huyo na kuchukua hatua zaidi endapo haitatekelezwa ipasavyo.




