Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeAfyaUmmy: Samia amewatendea haki wenye ulemavu

Ummy: Samia amewatendea haki wenye ulemavu

Moshi, Oktoba 1, 2025 – Mbunge mteule wa Viti Maalum kwa Watu Wenye Ulemavu na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewatendea haki watu wenye ulemavu na amewaomba Watanzania kumpa kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, Moshi, Nderiananga alisema tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021, Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanapata huduma muhimu bila vikwazo.

Alisema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya upatikanaji wa mafuta ya kupaka kwa albino, ambapo awamu ya kwanza Sh milioni 60 zilitolewa na zaidi ya watu 5,000 wamenufaika.

“Rais Samia ameonyesha utu na kuwatendea haki watu wenye ulemavu kwa kuwateua na kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi serikalini. Serikali yake haibagui, inamjali kila mmoja,” alisema.

Akiwaomba wananchi wa Moshi na Watanzania kwa ujumla kumpa kura Rais Samia ifikapo Oktoba 29, Nderiananga alisema:
“Utu unalipwa kwa wema, na sisi tutakulipa bila wasiwasi.”

Aidha, alisema Rais Samia amewekeza katika elimu ya watoto wenye ulemavu kwa kujenga mabweni 188 nchi nzima, ikiwemo moja katika Wilaya ya Moshi lililojengwa kwa Sh milioni 80.

“Kabla ya Rais Samia, wanafunzi wenye ulemavu walikosa mabweni na kukabiliwa na changamoto nyingi. Sasa wana mazingira bora ya kujifunza kama watoto wengine,” alisema.

Vilevile, Nderiananga alibainisha kuwa Serikali imejenga ofisi maalum za watu wenye ulemavu mjini Dodoma kwa gharama ya Sh milioni 34, jambo ambalo halikuwepo kabla ya awamu ya sita.

Aliongeza kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi wa maeneo mbalimbali wakati wa majanga kwa kutoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 7 nchi nzima.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments