Profesa wa somo la Anatomia katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Ngasapa, amezindua mfululizo wa vitabu vitano vya taaluma ya Human Anatomy vinavyolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa udaktari nchini na kanda ya Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo, Profesa Ngasapa amesema wazo la kuandika vitabu hivyo limetokana na uzoefu wake wa zaidi ya miaka 45 ya kufundisha chuoni hapo, ambapo alibaini upungufu mkubwa wa vitabu vya rejea, hususan vinavyoendana na mahitaji ya wanafunzi wa Tanzania.
Ameeleza kuwa zamani vitabu vilikuwepo kwa uchache, lakini kwa sasa havipatikani kabisa, hali iliyowalazimu wanafunzi kutegemea notsi za walimu ambazo hutofautiana kutoka mhadhiri mmoja hadi mwingine. Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi walihitimu bila kuwa na kitabu maalum cha rejea kwa matumizi yao ya baadaye.
“Wanafunzi wetu wanategemea notsi tu. Wakimaliza masomo wanaondoka nazo, na wakati mwingine hupotea. Hawana kitabu cha msingi cha kurejea wanapokuwa kazini,” amesema Ngasapa




Sababu nyingine iliyomsukuma kuandika vitabu hivyo ni ugumu wa lugha iliyotumika katika vitabu vya zamani vilivyoandikwa na waandishi ambao Kiingereza ni lugha yao ya kwanza. Amesema vitabu hivyo viliandikwa kwa mazingira ya wanafunzi wa Ulaya na Marekani, tofauti na wanafunzi wa Tanzania ambao Kiingereza ni lugha ya tatu, hali inayowafanya wapate ugumu kuelewa maudhui.
Aidha, ameeleza kuwa mifano iliyotumika katika vitabu vya zamani haikuendana na mazingira ya hapa nchini. Ametolea mfano maelezo ya mfuko wa nyongo kufananishwa na aina ya peas (njegere) zinazopatikana Ulaya, tofauti na zinazofahamika kwa wanafunzi wa Tanzania.
Prof. Ngasapa ameongeza kuwa vitabu vya zamani vilihamasisha zaidi kukariri badala ya kuelewa, huku mitaala ya sasa ikizingatia mfumo wa elimu unaozingatia umahiri (Competency-Based Education). Hivyo, vitabu alivyoviandaa vinaendana na mfumo huo kwa kumsaidia mwanafunzi kuelewa na kutumia maarifa kwa vitendo badala ya kukariri.
Amefafanua kuwa mchakato wa kuandika vitabu hivyo umechukua muda mrefu, ukiambatana na majukumu ya kufundisha na kufanya utafiti. Amelazimika pia kuandaa michoro na picha nyingi kwa kuwa somo la Anatomia linahitaji vielelezo vya kuona, jambo lililoongeza changamoto katika uandishi.
Vitabu hivyo vinajumuisha maeneo mbalimbali ya mwili wa binadamu, kuanzia muundo unaoonekana kwa macho (gross anatomy), muundo unaoonekana kwa kutumia darubini, hadi maendeleo ya kiumbe tumboni kuanzia utungaji wa mimba hadi kuzaliwa. Pia kuna kitabu maalum kwa wanafunzi wa afya ya kinywa na meno kinachochambua kwa undani muundo wa meno na taya.
Amesema lengo lake lilikuwa kuandaa mkusanyiko kamili wa vitabu vinavyoshughulikia kwa mapana somo la Anatomia, badala ya kuandika kitabu kimoja na kuacha mapengo katika maeneo mengine.
Kuhusu upatikanaji, Prof. Ngasapa amesema vitabu hivyo vinamilikiwa kisheria na yeye, lakini vimechapishwa kwa ufadhili wa chuo. Vitauzwa kwa gharama nafuu inayolenga kufidia uzalishaji ili kuwezesha uchapishaji wa nakala zaidi bila kuendelea kutegemea ufadhili wa chuo.

Amebainisha kuwa tayari kuna maombi kutoka nchi za Zambia, Zimbabwe, India na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, akieleza kuwa changamoto ya upungufu wa vitabu vya Anatomia ni ya kikanda.
Kwa upande wa uendelevu wa taaluma, Prof. Ngasapa amesema amekuwa akiwajengea uwezo wahadhiri vijana watakaokuja kuendeleza kazi hiyo.
Akizungumzia mchango wa vitabu hivyo, amesema vitasaidia kuboresha ufundishaji wa madaktari nchini kwa kuwa Anatomia ni msingi wa taaluma ya udaktari. “Mwanafunzi lazima auelewe mwili wa binadamu kwa kina kabla ya kwenda kliniki au kufanya upasuaji,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Rais wa Ndaki ya Tiba MUHAS, Profesa Agricola Johakim, amesema chuo kinajivunia kuwa na mhadhiri mwenye kujituma kama Prof. Kasapa. Ameeleza kuwa uandishi wa vitabu ni sehemu ya majukumu ya kitaaluma ya chuo, na kwamba vitabu hivyo vitawasaidia sana wanafunzi kupata elimu bora kwa lugha rahisi na inayoeleweka.




