Wajasiriamali wadogo 50 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo ya urejeleshi katika sekta za mazingira na kilimo, yatakayowasaidia kuboresha mfumo wa usindikaji, uchakataji, kuongeza kipato na kutengeneza ajira.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Anza, Joshua Silayo, alisema mpango huo unalenga kuwajengea uwezo vijana kutumia fursa zilizopo kwenye taka, hususan plastiki, kama njia ya kujiongezea kipato sambamba na kuhifadhi mazingira.
Silayo alisema biashara za urejeleshi zinahimiza matumizi sahihi ya rasilimali kwa kuzitumia zaidi ya mara moja au kuhuisha bidhaa kwa matumizi mengine, hivyo kupunguza taka na kutatua changamoto za kimazingira.

Aidha, alibainisha kuwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya biashara, mitaji midogo na kuwatafutia wajasiriamali mitandao ya masoko na uwekezaji. Aliongeza kuwa asilimia 80 ya walengwa wa programu zao ni vijana na wanawake kutokana na uhitaji mkubwa wa kuwajengea uwezo katika jamii.
Kwa niaba ya washiriki, Laetus Buberwa, alisema amebuni biashara ya Nishati-Mix ambapo hutumia makopo na mabomba ya plastiki kuzalisha nishati safi ya kupikia. Alisema teknolojia hiyo ni mbadala wa kuni na mkaa, ambavyo ni hatarishi kiafya na vinachangia uharibifu wa mazingira.
Naye Kelvin Majula, Mratibu wa Mradi wa Urejeleshi, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana kufanya uchumi jumuishi utakaowanufaisha wao na jamii inayowazunguka, huku programu ikizingatia miundo ya biashara zao.





