Saturday, December 6, 2025
spot_img
HomeBiasharaVi Agroforestry kuadhimisha miaka 10 ya maonesho ya kilimomisitu Musoma

Vi Agroforestry kuadhimisha miaka 10 ya maonesho ya kilimomisitu Musoma

Shirika la Maendeleo la Kiswidi Vi Agroforestry, linalotekeleza miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, limeandaa maonesho ya 10 ya kilimomisitu yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma kuanzia Novemba 13 hadi 15 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mkazi wa shirika hilo nchini, Martha Olotu, alisema maonesho hayo yatafanyika katika Kituo cha Mafunzo cha Kilimomisitu kilichopo Bweri, Musoma, na yanatarajiwa kuwaleta pamoja zaidi ya washiriki 6,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Olotu, tukio hilo litakuwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 15 ya mafanikio ya shirika hilo katika kutekeleza miradi ya matumizi endelevu ya ardhi, usalama wa chakula, na ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akifafanua zaidi, alisema maonesho hayo yatabebwa na kaulimbiu isemayo “Kilimomisitu kwa ukuaji jumuishi na endelevu,” ambapo yatafungua jukwaa la kitaifa la kubadilishana maarifa, mijadala ya kisera na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya kilimo.

“Maonesho haya yatawakutanisha wakulima, watafiti, watunga sera, wabia wa maendeleo na sekta binafsi kwa lengo la kuhamasisha kilimomisitu nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Olotu.

Aidha, alibainisha kuwa maonesho hayo yataonesha mchango wa kilimomisitu katika kuboresha maisha ya wakulima wadogo, kuhifadhi bayoanuai, kuongeza usalama wa chakula na kipato cha kaya, sambamba na kutafuta suluhisho kwa changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Olotu alisema maonesho hayo yatakuwa na programu ya siku tatu yenye mijadala na uwasilishaji wa mada katika maeneo makuu matatu:

  1. Fursa za kiuchumi vijijini zinazozingatia vyanzo mbalimbali vya mapato na minyororo ya thamani jumuishi.
  2. Mifumo ya ikolojia na uhifadhi wa bayoanuai kwa ajili ya ustahimilivu wa tabianchi na afya ya udongo.
  3. Mazinga ya kisera na kifedha yanayorahisisha utekelezaji wa mifumo jumuishi ya kilimo na usalama wa umiliki wa ardhi.

Aliongeza kuwa maonesho hayo pia yatashirikisha mashirika ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa, hatua itakayoongeza nguvu ya ushirikiano katika kukuza kilimo jumuishi na kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Katika kuelekea maonesho hayo, kutakuwa na kampeni ya upandaji miti itakayofanyika katika Shule ya Msingi Mkiringo, Musoma, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama. Kampeni hiyo itahusisha watumishi wa Vi Agroforestry, washirika wa zamani na wa sasa, wakulima, wanafunzi, walimu na wageni waalikwa.

“Ushirikiano huu unaonyesha namna kilimomisitu kinavyoweza kusaidia kurejesha mifumo ya ikolojia, kuimarisha uhimilivu wa jamii, na kuhusisha vijana kama chachu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi,” alisema Olotu.

Aidha, alitoa wito kwa wadau wa sekta binafsi na ya umma kuungana kusherekea safari ya miaka 10 ya maonesho hayo na mchango wake katika kuboresha maisha ya Watanzania.

“Viongozi wa kijamii, maafisa wa serikali, watafiti na washirika wa sekta binafsi wanahimizwa kushiriki, kubadilishana maarifa, na kujadili mikakati ya kisera itakayowezesha kilimomisitu kuendelea kuchangia ukuaji jumuishi na endelevu nchini,” alisisitiza Olotu.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments