Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewapa kitita cha mamilioni vijana tisa walioshinda shindano la kubuni na kuandika namna Mamlaka hiyo inavyoweza kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi na mapato.
Hafla ya kuwakabidhi fedha hizo imefanyika leo katika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Fedha, Khamis Musa Omari.
Hubayb Said aliyependekeza program ya simu itakayotoa vikumbusho vya kodi kwa njia ya taarifa za papo kwa papo alizawadiwa shilingi milioni 20.
Isamael Mkumbi aliyebuni mfumo unaopendekeza matumizi ya teknolojia ya blockchain kuhifadhi taarifa za walipa kodi na miamala kwa usalama zaidi alipewa shilingi milioni 20, ngao na cheti.




Ajra Noordini aliyebuni namna ya kuoanisha na kuendesha kiotomatiki nyaraka za uhasibu kama Credit Notes kama sehemu ya kuongeza uwazi alizawadiwa shilingi milioni 20, ngao na cheti
Erick Joachim aliyebuni ubunifu unaopendekeza mfumo utakaoweza kuandaa rasimu ya matokeo ya ukaguzi wa kodi kiotomatiki kwa kulinganisha taarifa za mauzo, manunuzi, PAYE, na zuio la kodi alizawadiwa shilingi milioni 20.
Ng’wang’wa Loyani aliyebuni ubunifu unaopendekeza matumizi ya dola za Marekani kwa watumiaji wa simu za kawaida, roboti za mawasiliano kwenye whatsap na Teregram pamoja na program yenye mfumo wa michezo alizawadiwa shilingi milioni 20.

Malehe Masubi aliyebuni ubunifu unaopendekeza matumizi ya zana za automation na akili mnemba kurahisisha kazi zinazojirudia, kupunguza makosa mbalimbali ya kibinadamu na kuongeza tija alizawadiwa shilingi milioni 30.
Emma Sambaya aliyebuni wazo linalopendekeza kuunganisha mfumo wa stakabadhi za EFD na mfumo wa NHIF ili sehemu ya VAT ichangie moja kwa moja kwenye bima ya afya ya mlipakodi alipewa milioni 30.
Edmund Komba aliyebuni matumizi ya QR Code na ufuatiliaji wa GPS ili kubaini bidhaa bandia na zisizolipiwa kodi kwa wakati halisi alipewa Sh. milioni 30.
Gabrieli Mshenene ambaye alibuni mfumo wa kidijitali unaolenga kupambana na Ankara bandia na udanganyifu wa uingizaji wa bidhaa kwa kufanya uhakiki wa taarifa za mizigo na Ankara kwa wakati halisi alivuna Sh. milioni 50.






