Saturday, February 28, 2026
spot_img
HomeAfyaWanawake Viongozi wachangia milioni 30 kuokoa watoto wenye matatizo ya moyo

Wanawake Viongozi wachangia milioni 30 kuokoa watoto wenye matatizo ya moyo

‎Washiriki wa Programu ya Mwanamke Kiongozi inayoendeshwa na Chama cha Waajiri Tanzania  (ATE) wamekabidhi mchango wa Sh milioni 30 kwa Heart Africa Foundation ili kusaidia matibabu ya watoto saba wenye matatizo ya moyo wanaohudumiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Mchango huo umetolewa kama sehemu ya mafunzo ya uongozi kwa vitendo kwa washiriki wa darasa la 11 la programu hiyo, inayolenga kuwajengea uwezo wanawake kuwa viongozi imara, waadilifu na wanaorejesha kwa jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Februari 28,2026, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzan Doran Ndomba, amesema Programu ya Mwanamke Kiongozi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuwaandaa wanawake katika maeneo ya uongozi, usimamizi wa taasisi na uwajibikaji wa kijamii. Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya wanawake 600 kutoka sekta mbalimbali – wakiwemo wabunge wa Tanzania Bara na visiwani na viongozi wa taasisi binafsi na za umma  wamenufaika na mafunzo hayo.

Amesema hatua hiyo ni sehemu muhimu ya kuwajengea washiriki uwezo wa kuwa viongozi wanaogusa maisha ya jamii inayowazunguka.

“Tunafundisha si tu namna ya kuwa viongozi katika nafasi zao, bali pia umuhimu wa kurudisha kwa jamii. Leo washiriki wetu wameonesha kwa vitendo maana ya uongozi wenye kugusa maisha ya watu,” amesema Suzan, akitoa pongezi kwa HTAF, JKCI na wadau wote waliofanikisha tukio hilo.

Kwa upande wake, Esther Christopher Mwabuwilo, Rais wa Programu ya Mwanamke Kiongozi Cohort 11, amesema waliguswa na hali ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo, hasa familia zinapokabiliwa na gharama kubwa za matibabu.

Ameelezea Programu ya Female Future, kuwa programu hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kuwa viongozi imara katika nyanja mbalimbali za maisha na kazi. Alisisitiza kuwa, kama wanawake na wazazi, wanayo dhamira ya dhati ya kusaidia watoto wenye changamoto za moyo, kwa vitendo na kwa kugusa maisha ya walio katika uhitaji.

“Gharama za upasuaji wa moyo zinaweza kufikia kati ya Sh milioni 8 hadi 16 au zaidi. Kwa familia nyingi hizi ni fedha kubwa. Tuliona ipo haja ya kushirikiana kuokoa maisha ya watoto hawa. Kwa kushirikiana na HTAF, tumechagua CSR ya mwaka huu kurejesha kwa jamii hapa JKCI. Tunakabidhi takribani milioni 30 zitakazowezesha watoto 7 kupata matibabu na maisha mpya” ,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, amewashukuru washiriki hao kwa mchango huo akieleza kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika vifaa na wataalamu, bado baadhi ya wagonjwa hushindwa kumudu gharama za matibabu.

“Taasisi ilianzishwa rasmi mwaka 2015. Hadi sasa, asilimia 60 ya uongozi wa JKCI ni wanawake, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya afya na uongozi.Kwa sasa, JKCI ina matawi 7 nchini, ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuokoa maisha na kuboresha huduma za moyo kwa Watanzania.Ushirikiano huu na Programu ya Mwanamke Kiongozi Kundi la 11 chini ya Chama cha Waajiri Tanzania ni ushuhuda wa nguvu ya uongozi wa wanawake katika kuleta mabadiliko chanya na endelevu kwa jamii.” amesema Dk. Kisenge 

Amesema kuwa kuanzishwa kwa Heart Team Africa Foundation kulilenga kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo ambao hawana uwezo wa kifedha kupata matibabu. Tangu kuanzishwa kwake, Taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 2, na kusaidia zaidi ya watoto 300 kupata matibabu ya moyo, hivyo kuokoa na kubadilisha maisha ya wengi wao.

 Amesisitiza pia umuhimu wa kaulimbiu ya “Jua Namba Zako Kiafya” kama njia ya kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa.

Katika kuonesha kuthamini mchango huo, ametangaza utoaji wa huduma za afya bila malipo kwa wahitimu wa Programu ya Mwanamke Kiongozi Kundi la 11.

Dk. Nice Majani, Daktari Bingwa wa Moyo wa Watoto na Mtendaji Mkuu wa HTAF, amesema mchango huo utawezesha watoto saba waliokuwa kwenye orodha ya kusubiri kupatiwa upasuaji na kurejea katika maisha ya kawaida. Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015, imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 2 na kusaidia zaidi ya watoto 300 kupata matibabu ya moyo.

“Pongezi za dhati kwa washiriki wote wa Programu ya Mwanamke Kiongozi. Tunayofuraha pia kuwakaribisha washiriki na wahitimu wa Programu ya Mwanamke Kiongozi kupata huduma bila malipo  katika kituo chetu cha JKCI Oysterbay chenye huduma za kisasa zaidi kama ilivyoagizwa na Dk. Peter Kisenge.Nitoe shukrani kwa mchango wenu wa milioni 30 ni mkubwa sana unarejesha matumaini, unatoa nafasi kwa watoto kuishi, kucheza na kufurahia maisha.” Dk. Majani.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments