Monday, March 23, 2026
spot_img
HomeHabariWasichana 150 wanufaika na kambi ya TEHAMA ya TGEE 2026

Wasichana 150 wanufaika na kambi ya TEHAMA ya TGEE 2026

Wasichana 150 kutoka mikoa 20 nchini wananufaika na mafunzo ya Kambi ya Teknolojia ya TGEE 2026, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia ili kuboresha maisha yao na kuongeza kipato.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) – Kijitonyama, yamewaleta pamoja washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiwemo kutoka mikoa ya pembezoni, ili kupata ujuzi wa kisasa unaohitajika katika soko la ajira.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa Uendelezaji TEHAMA na Utafiti kutoka Tume ya TEHAMA, Jasson Ndaguzi, amewahimiza wanawake kujifunza na kutumia teknolojia kwa ufanisi ili kuongeza thamani ya kazi zao za kila siku na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yatawasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi na kufungua fursa mbalimbali za ajira na ubunifu katika sekta tofauti.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Help to Help Academy East Afrika, Hepifania Mhagama, amesema kuwa mradi huo una zaidi ya miaka 11 na umekuwa ukilenga kupunguza pengo la ujuzi wa kidijitali miongoni mwa vijana, hasa wanawake.

Ameeleza kuwa vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu hukosa ujuzi wa vitendo katika matumizi ya teknolojia, hali inayowafanya kushindwa kuhimili ushindani katika soko la ajira.

“Programu hii inalenga kuwajengea uwezo washiriki kutambua na kutumia fursa za kidijitali, na tunatarajia watakuwa mabalozi wazuri katika familia na taifa kwa ujumla,” amesema Mhagama.

Aidha, taasisi ya Help to Help East Afrika kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoka Sweden, imeendelea kutoa mafunzo ya kidijitali kwa makundi maalum ya wanawake na wasichana kutoka mikoa mbalimbali pamoja na vyuo vikuu nchini.

Mafunzo hayo yanajikita katika kuwapatia washiriki ujuzi wa vitendo wa TEHAMA, uwezo wa kutatua changamoto, pamoja na uongozi, kwa lengo la kuwabadilisha kutoka watumiaji wa kawaida wa teknolojia hadi kuwa wabunifu na viongozi katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu, bado kuna changamoto ya pengo la kidijitali kati ya jinsia ambapo wanawake wana upatikanaji mdogo wa intaneti kwa asilimia 43 ukilinganishwa na wanaume katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Pia, takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya waajiri hawaridhishwi na kiwango cha ujuzi wa TEHAMA kwa wahitimu, huku ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo ukiendelea kuwa mdogo licha ya ukuaji wake mkubwa nchini Tanzania.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Sharom Peter, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, amesema fursa hiyo itamwezesha kujifunza zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia na namna ya kukabiliana na changamoto za maisha.
Amesema anatarajia kutumia maarifa atakayopata kujikwamua kiuchumi na kujiendeleza katika nyanja mbalimbali za teknolojia.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana na wanawake, kwa kuwajengea kujiamini, ubunifu, na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments