Nianze kwa kutoa pongezi za dhati kwa Watanzania wote kwa kutekeleza kwa uaminifu na uzalendo maelekezo ya Serikali yaliyowataka Jumanne, Desemba 9, 2025, Siku ya Uhuru wa Tanganyika wa kuadhimisha sikukuu hiyo wakiwa katika makazi yao.
Hatua hii imeonesha ukomavu wa kiakili na kiutashi wa wananchi katika kulinda amani, utulivu na maslahi mapana ya Taifa letu na kukataa vishwawishi vya kufanya maandamano ambayo Jeshi la Polisi iliyapiga marufuku Desemba 5, kwa sababu yamekosa sifa kisheria.
Uamuzi wa Serikali kutoa maelekezo hayo ulitokana na kuwapo kwa taarifa na tetesi za maandamano yasiyo na ukomo, yaliyokuwa yakiratibiwa na kuhamasishwa kiupitia mitandao ya kijamii.
Katika mazingira ya sasa ya utandawazi, taarifa potofu na uchochezi huenea kwa kasi, lakini suala la usalama wa raia na utulivu wa nchi linapewa uzito wa kipekee na Serikali.
Hatua ya Watanzania wengi kutoshiriki au kujihusisha na maandamano hayo ni ishara ya kuliheshimu Taifa, kulinda amani yetu ya muda mrefu, na kutanguliza maslahi ya nchi kuliko kuvunja amani ya nchi, kwa maslahi ya watu wachache. Huu ni ushahidi kuwa Watanzania wanaelewa thamani ya utulivu na madhara ya amani ikitoweka.
Ni wazi kuwa tukio la vurugu lililotokea kuanzia Oktoba 29 lilikuwa somo muhimu kwa Taifa. Vurugu hizo, zilizosababishwa na watu wachache wasiotakia mema nchi yetu, ziliathiri kwa kiasi kikubwa mtiririko wa maisha ya wananchi.
Kwa takribani siku tano, shughuli za kiuchumi, kijamii na hata kisaikolojia zilipata msukosuko mkubwa kutokana na hali ya hofu na kutokuwa na uhakika. Haya ni madhara ambayo raia wa kawaida hasa wa kipato cha chini wanaotegemea kipato cha kila siku hukumbana changamoto hiyo.
Ndiyo maana wakati naanza uchambuzi huu nilitoa pongezi Watanzania walionyesha kwa vitendo kuwa hawapo tayari kurudia makosa ya nyuma, na wamekataa maandamano ambayo kwa mara nyingine yangeweza kuharibu taswira ya Taifa letu, kuvuruga utulivu na kuathiri shughuli za kiuchumi kwa mamilioni ya watu.
Zaidi ya hayo Watanzania wameonyesha kuwa utamaduni wa Kitanzania si wa vurugu, bali wa mazungumzo, utulivu, undugu na kuheshimu misingi ya amani iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili.
Mwisho, navipongeza kwa dhati vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha ulinzi kabla, wakati na baada ya Desemba 9. Uwepo wao, na namna walivyodhibiti taarifa za taharuki, umeongeza imani kwa wananchi na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.
Hatua hii imeonesha kwa mara nyingine umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya usalama na wananchi katika kulinda msingi muhimu zaidi wa maendeleo na amani.




