Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushirikiana kwa karibu na wenyeviti wa mitaa ili kutatua changamoto za maji na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mamlaka hiyo.

Akizungumza leo, Februari 18, na Wenyeviti wa Mitaa wa Wilaya ya Kinondoni, Waziri Aweso amewasihi viongozi wa mitaa kushirikiana na DAWASA kwa karibu, huku akiitaka DAWASA nayo kuwapa ushirikiano wenyeviti hao.
“Niwaombe sana Wenyeviti wa mitaa tuwape ushirikiano DAWASA na pia niwaombe DAWASA muwape ushirikiano Wenyeviti,” amesema Aweso.
Ameelekeza pia kuwa DAWASA ihakikishe inashiriki mikutano ya wenyeviti wa mitaa ili kusikiliza na kutatua changamoto za maji katika maeneo yao.




“Muwape ushirikiano, muwe na mawasiliano yao. Wakipiga simu muwape taarifa, wakiwaita kwenye mkutano, hakikisheni mwakilishi wa DAWASA yupo kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo,” amesisitiza Waziri.
Aidha, Aweso ameitaka DAWASA kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za haraka kuhusu hitilafu na matengenezo ili kuepusha sintofahamu na upotoshaji wa taarifa.




“Wakati mwingine zipo hitilafu zinajitokeza, niwasihi sana zinapotokea viongozi wasizijue kupitia mitandao, bali wapeni taarifa wenyeviti mapema,” ameongeza.
Pamoja na hayo, Waziri Aweso ameipongeza DAWASA kwa kuwa ya kwanza kutekeleza agizo lake la kuwataka viongozi wa mamlaka za maji nchini kukutana na wenyeviti wa mitaa na kushirikiana nao katika kutatua changamoto za maji na kutekeleza miradi ya maji nchini.



