Simanzi imetanda nyumbani kwa Dk. Mabula Mahande, mkazi wa Uzunguni jijini Mbeya, wakati wa kuaga mwili wa binti yake Shyrose Mahande (21), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Mbeya.
Shyrose alitoweka Septemba 14 baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana, na Septemba 16 mwili wake ulipatikana eneo la Nane Nane ukiwa umeteketezwa kwa moto. Tukio hilo lilileta vilio kwa wanafamilia, wananchi na wanafunzi wenzake.
Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, imeliita tukio hilo la kinyama na kuagiza polisi kufanyakazi usiku na mchana kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Itashangaza kuona watu wa namna hii wanabaki mitaani. Ni wajibu wa kila mmoja kukemea matukio haya ya kikatili,” alisema Itunda.
Baada ya kuagwa nyumbani kwao na ibada maalum katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, mwili wa marehemu ulizikwa katika makaburi ya Iwambi








