Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeBiasharaAirtel Africa, Nokia kuunda mtandao mkubwa wa fiber barani Afrika

Airtel Africa, Nokia kuunda mtandao mkubwa wa fiber barani Afrika

Cape Town, Novemba 2025 — Airtel Africa, mmoja wa watoa huduma wakubwa wa mawasiliano na huduma za fedha kwa njia ya simu katika nchi 14 barani Afrika, imemteua Nokia kujenga mtandao wa kisasa wa mkongo wa mawasiliano wa ardhini (terrestrial fiber) kupitia huduma yake ya Airtel Africa Telesonic.

Mradi huo wa kimkakati unalenga kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati na kuzifikisha moja kwa moja kwenye mkongo wa mawasiliano wa baharini na ardhini. Hatua hii itaboresha upatikanaji wa huduma za intaneti kwa ubora wa juu, uhakika na gharama nafuu, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa kijamii barani Afrika.

Mradi huu umetangazwa katika Mkutano wa 28 wa AfricaCom, jukwaa kubwa duniani linalowakutanisha viongozi wa sekta ya mawasiliano wanaolenga soko la Afrika. Kupitia mradi huo, mkongo wa 2Africa utaunganishwa moja kwa moja na miundombinu ya ardhini, na kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa kasi na uweledi wa juu.

Kwa kutumia teknolojia ya Nokia 1830 Photonic Service Switch (PSS), mtandao huo mpya utaweza kubeba hadi 38 Terabiti kwa sekunde (38 Tbps). Teknolojia hiyo imeundwa kuwa tayari kupokea maboresho ya C+L Band kwa ajili ya kuongeza uwezo wa mtandao. Mtandao wa DWDM unaojengwa utakuwa na nodi 139 zinazounganisha nchi mbalimbali, na utaendeshwa na mifumo ya kisasa ya Nokia ya Photonic Service Engine (PSE) yenye ubora na kasi ya juu.

Zaidi ya kuboresha miundombinu ya kimtandao, mradi huu unaonesha dhamira ya Telesonic kuwawezesha wafanyabiashara, sekta ya elimu na afya kupata huduma bora za kidijitali zenye ufanisi zaidi.

Razvan Ungureanu, Afisa Mkuu wa Teknolojia wa Airtel Africa, amesema:
“Utekelezaji wa Nokia 1830 PSS ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya mtandao barani Afrika. Teknolojia hii inatuwezesha kuongeza uwezo wa mtandao na kutoa huduma za kasi ya juu ili kukidhi mahitaji makubwa ya intaneti.”

Naye PD Sarma, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa Telesonic, amesema:
“Ushirikiano wetu na Nokia ni hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali barani Afrika. Mtandao huu utaendesha ukuaji wa uchumi, kuwawezesha wananchi na kufungua fursa mpya kwa biashara na watu binafsi.”

Kwa upande wake, Samer Lutfi kutoka Nokia amesema:
“Tunajivunia kushirikiana na Airtel Africa Telesonic kwenye mradi huu mkubwa. Teknolojia yetu ya DWDM yenye uwezo mkubwa imeundwa kusaidia taasisi na biashara kusukuma mbele mageuzi ya kidijitali na kukuza uchumi wa eneo.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments