Sunday, November 2, 2025
spot_img
HomeBiasharaCRDB, BPIFrance waipa SMZ bil. 115/- kusimamia ardhi

CRDB, BPIFrance waipa SMZ bil. 115/- kusimamia ardhi

KATIKA kuunga mkono juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Taasisi ya Fedha ya Ufaransa (BPI France) imetia saini mkataba wa kuikopesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kiasi cha Euro milioni 37.5 (sawa na Sh. bilioni 115) kwa ajili ya kufunga Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Taarifa za Ardhi (LARIS).

Mkopo huo unatarajiwa kuondoa changamoto zilizopo katika sekta ya ardhi, hususan migogoro ya umiliki. CRDB itatoa Euro milioni 7.949 na BPI France itatoa Euro milioni 29.55.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Ikulu Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wananchi, hivyo serikali imeamua kuimarisha usimamizi wake kwa njia ya kidijitali.

“Ninawashukuru Benki ya CRDB kwa kutuunga mkono katika wazo hili. Serikali inaweka mazingira rafiki kwa kila mwananchi kunufaika na ardhi anayoimiliki. Baada ya kufunga mfumo huu wa LARIS, taarifa zote za umiliki na usimamizi wa ardhi zitapatikana kirahisi na kuondoa migogoro ya mipaka na matumizi,” alisema Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwa kumaliza migogoro ya ardhi kupitia mifumo ya kidijitali kutawapa wananchi fursa ya kutumia ardhi zao kama dhamana ya mikopo kwa taasisi za fedha, hivyo kuongeza kasi ya maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Khadija Khamis Rajab, alisema mfumo huo utasaidia pia serikali katika utambuzi wa wamiliki wa ardhi na ukusanyaji wa kodi. “Pindi mfumo huu utakapoanza kufanya kazi, makusanyo ya kodi ya ardhi yataongezeka na serikali itapata mapato yote kwa wakati,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema mfumo huo utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi Zanzibar kwa kuweka misingi imara ya usimamizi na umilikishaji wa ardhi kwa njia ya kidijitali.

“Mradi huu utafungua fursa mpya za kifedha na kiuchumi kwani urasimishaji wa ardhi utajenga imani kwa taasisi za fedha kutoa mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa wananchi,” alisema Nsekela.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itachochea ustawi wa wananchi kupitia uboreshaji wa huduma, ukuaji wa uwekezaji na ujenzi wa uchumi shirikishi.

Nsekela alisema katika mkakati wa biashara wa muda wa kati wa 2023–2027, CRDB imeweka kipaumbele katika ushirikiano wa kimataifa ili kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo. Alibainisha kuwa benki hiyo imeshiriki katika miradi mikubwa kama ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Reli ya Kisasa (SGR), na Zanzibar imepata zaidi ya Sh. bilioni 484 kwa miradi ya barabara, shule na Uwanja wa Ndege wa Pemba.

Aidha, alisema CRDB imekuwa kinara katika ubunifu wa huduma na bidhaa kama hatifungani za kijani na hatifungani ya miundombinu ya Samia Infrastructure Bond, zilizokusanya zaidi ya Sh. bilioni 494 kwa ajili ya miradi ya kijani na miundombinu.

“Hivi karibuni pia tumetoa hatifungani ya CRDB Al Barakah Sukuk iliyotuwezesha kukusanya Sh. bilioni 125.4 na dola milioni 32.3 za Marekani. Fedha hizi zinalenga kuchochea maendeleo katika sekta za ujasiriamali, biashara, kilimo, uvuvi, elimu, afya, utalii na miradi mingine ya kimkakati,” alisema Nsekela.

Makamu wa Rais anayesimamia Mikopo ya Nje wa BPI France, Alienor Daugreilh, alisema taasisi hiyo imeamua kushirikiana na Zanzibar kutokana na imani juu ya uimara wa uchumi wa visiwa hivyo.

“Huu ni mwanzo tu. BPI France itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufanikisha miradi ya maendeleo. Tukiwa na wadau kama CRDB, tunaamini tunaweza kufanya mambo makubwa kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema Daugreilh.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments