Benki ya CRDB imezindua rasmi Ofisi yake ya Uwakilishi jijini Dubai, katika hafla iliyofanyika jana katika Hoteli ya kifahari ya Intercontinental, Dubai.
Uzinduzi huo uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.






Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo ameipongeza Benki ya CRDB kwa hatua hiyo muhimu, akisema inaiweka Tanzania pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika nafasi ya kimkakati ndani ya uchumi wa pamoja unaokadiriwa kufikia takribani dola za Marekani bilioni 800.





Amesema hatua hiyo inaunganisha moja kwa moja ukanda huo na mifumo ya mitaji ya kimataifa, huku CRDB ikifanya kazi kama daraja kati ya fursa za kikanda na masoko ya fedha ya dunia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema Ofisi ya Uwakilishi ya Dubai itatumika kama jukwaa la kimkakati la kuwezesha biashara, kuvutia wawekezaji na kuchochea upatikanaji wa mitaji ya kimataifa kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 700 wakiwemo viongozi waandamizi wa Serikali, wawekezaji wa kimataifa, taasisi za fedha za kimataifa pamoja na washirika wa maendeleo.
Ushiriki huo mkubwa unaashiria kuongezeka kwa imani ya kimataifa kwa Benki ya CRDB kama kiungo muhimu kati ya Afrika na masoko ya fedha ya kimataifa.








