Utafiti uliofanywa mwaka 2025 na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika mikoa 10 nchini umebaini kuwa wanaume wanaongoza kwa unywaji wa pombe kupita kiasi kwa asilimia 82, huku wanawake wakiwa asilimia 18.
Akizungumza leo Januari 21, 2026 jijini Dodoma, Ofisa Udhibiti Ubora Mkuu wa TBS Makao Makuu, Moses Mbambe, amesema matokeo hayo yalipatikana kupitia utafiti uliohusisha watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 60 kutoka makundi mbalimbali ya jamii.
Mbambe alikuwa akitoa elimu kwa waendesha bodaboda na wafanyabiashara katika Soko la Sabasaba, ambapo alieleza kuwa utafiti huo umebaini kuwa wanaume ndio wanaoongoza kwa matumizi ya pombe kupita kiasi hapa nchini.
Alitaja mikoa iliyotumika katika utafiti huo kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Manyara, Dodoma, Songwe, Kigoma, Kilimanjaro na Mtwara.
Mbambe alisema aina za pombe kali ndizo zinazoongoza kwa kutumiwa kupita kiasi, zikifuatiwa na bia na mvinyo. Kutokana na hali hiyo, TBS imeamua kutoa elimu kwa makundi mbalimbali nchini ili kupunguza madhara yatokanayo na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Alieleza kuwa madhara ya unywaji huo ni pamoja na familia na jamii kupoteza nguvu kazi kutokana na uraibu wa pombe, pamoja na kusababisha ajali za barabarani hususan kwa madereva.
Awali, Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS Makao Makuu, Gwantwa Samson, alisema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuhamasisha unywaji wa pombe wa kistaarabu, sambamba na kuwashauri waraibu wa pombe kuacha kabisa matumizi yake ili kuepuka madhara makubwa kiafya na kijamii.
Aliongeza kuwa hadi sasa elimu hiyo imeshatolewa katika mikoa mitano ambayo ni Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Mwanza, huku mpango ukiwa ni kuendelea na mikoa mingine. Aidha, aliwasisitiza wananchi kuacha kutumia pombe za kienyeji ambazo hazijathibitishwa ubora wake.




