Dodoma Jiji yahamishia makao Babati

KLABU ya Dodoma Jiji imetangaza  itautumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati, mkoani Manyara katika mechi zake za nyumbani za Ligi Kuu kwa sasa wakati wakiufanyia marekebisho Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma.

Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga, aliliambia gazeti hili watatumia kama uwanja wake wa nyumbani na wataanza katika mchezo wao dhidi ya Namungo unaotarajiwa kuchezwa Septemba 12, mwaka huu.

Mpunga alisema marekebisho ya uwanja wa Jamhuri yanaendelea vizuri na wanaamini watarejea mapema Dodoma kuendelea na kampeni za kuwania taji hilo la Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tunacheza mechi zetu za Ligi Kuu mjini Babati kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa kipindi hiki, na tunaanzia mchezo dhidi ya Namungo, kama marekekebisho yataendelea basi mechi nyingine tunacheza tena hapo, lakini kama utakuwa tayari tutarejea kwenye uwanja wetu,” alisema Mpunga.

Bodi ya Ligi imeusimamisha Uwanja wa Jamhuri kutumika katika mchezo wa Ligi Kuu mpaka pale utakapokamilisha vigezo vinavyotakiwa.

Agosti 27, Bodi ya Ligi, ilitoa taarifa hiyo, ikisema kuwa uwanja huo umekosa ubora eneo la kuchezea’ ambapo sehemu kubwa ikiwa haina majani ya kutosha na yaliyopo ni dhaifu, jambo linalofanya usiwe salama kwa wachezaji, baada ya hilo ikaitaka Dodoma Jiji itafute uwanja mwingine hadi hapo utakapofanyiwa maboresho.

Dodoma Jiji imecheza mechi mbili mpaka sasa, lakini zote ikipoteza ugenini dhidi ya Mashujaa FC na kulazimishwa suluhu dhidi ya wenyeji Pamba Jiji.

Chanzo: Nipashe

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *