Thursday, March 5, 2026
spot_img
HomeHabariHizi hapa bidhaa na huduma ambazo wageni hawapaswi kuzifanya migodini

Hizi hapa bidhaa na huduma ambazo wageni hawapaswi kuzifanya migodini

 ▪️Ni utekelezaji wa maelekezo ya Mh Rais Samia juu ya ushiriki wa watanzania kwenye sekta ya madini

▪️Ni kupitia Marekebisho ya Kanuni ya Ushirikishwaji Watanzania Sekta ya Madini

▪️Manunuzi na Bidhaa Migodini  Yafikia Shilingi Trilioni 5 mwaka 2024

▪️Waziri Mavunde ataka Sekta Binafsi kuchangamkia fursa


📍 Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Madini imetangaza rasmi orodha ya huduma na bidhaa 20 zinazopaswa kutolewa migodini na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100, hatua inayolenga kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anayesisitiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini ili kuongeza manufaa ya rasilimali hizo kwa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Januari 5, 2025, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kufanyika marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za mwaka 2018.

Mhe. Mavunde amesema kuwa kwa awamu ya kwanza, tarehe 14 Novemba 2025, Tume ya Madini ilitangaza orodha ya huduma na bidhaa zinazopaswa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100, ambapo kwa mara ya kwanza Tume hiyo itakuwa ikitangaza orodha hiyo kupitia Kanuni ya 13A.

Akizungumzia mwenendo wa manunuzi, Waziri Mavunde amesema ununuzi wa huduma na bidhaa kutoka kwa kampuni za Kitanzania umeongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka Shilingi trilioni 1.85 kati ya jumla ya Shilingi trilioni 3.01 sawa na asilimia 62 mwaka 2018, hadi kufikia Shilingi trilioni 4.41 sawa na asilimia 88 ya jumla ya Shilingi trilioni 5.00 za manunuzi yaliyofanyika mwaka 2024.

Kwa upande wa ajira katika miradi ya madini, Waziri amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la ajira kwa Watanzania, kutoka ajira 6,668 kati ya ajira 7,003 sawa na asilimia 95 mwaka 2018, hadi ajira 18,853 kati ya ajira 19,356 sawa na asilimia 97 kufikia Desemba 2024.

Ameongeza kuwa katika nafasi zinazohitaji utaalamu wa juu unaoendana na ukuaji wa teknolojia duniani, Serikali imeweka utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania katika nafasi zinazoshikiliwa na wataalamu wa kigeni. Ameutaja Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation (Barrick Gold) kama mfano mzuri, ambapo nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na Watanzania kwa asilimia 100.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde amesema Serikali inaendelea kufungua wigo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini kwa kutenga eneo maalum la uwekezaji katika eneo la aliyekuwa Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi lenye ukubwa wa ekari 1,331. Eneo hilo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za migodini, ambapo tayari viwanda sita vimejengwa na wawekezaji 15 wameonesha nia ya kujenga viwanda zaidi.

Waziri Mavunde ameitaka sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa za usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma migodini ili kuhakikisha fedha nyingi zinabaki nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, amewasisitiza wawekezaji wote kuzingatia Sheria ya Madini pamoja na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania, huku akiwahimiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya madini kama njia ya kukabiliana na changamoto za ajira na kuongeza ustawi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments