Tuesday, February 17, 2026
spot_img
HomeAfyaHuduma za moyo bure zawafikia zaidi ya wananchi 1,200 Arusha

Huduma za moyo bure zawafikia zaidi ya wananchi 1,200 Arusha

Katika hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi, wakazi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wameanza kunufaika na huduma za vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo, mpango uliowezeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (Seliani).

Wananchi hao wametoa shukrani zao leo Jumanne, Januari 6, 2025, wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,CPA Amos Gabriel Makalla, aliyefika kukagua utekelezaji wa programu hiyo ya matibabu, ambayo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kupunguza gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Makalla aliishukuru JKCI kwa kuanzisha kituo chake ndani ya Hospitali ya Seliani, akisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Arusha, mikoa ya jirani pamoja na watalii wanaotembelea eneo hilo.

Aliongeza kuwa uwepo wa kituo hicho ni fursa muhimu kuelekea maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2027, ambapo Mkoa wa Arusha utakuwa miongoni mwa maeneo yatakayopokea wageni, mashabiki na washiriki wa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo, jumla ya wananchi takribani 1,200 tayari wamenufaika na huduma za vipimo na matibabu ya moyo bila malipo kupitia programu hiyo. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wananchi wasiokuwa na uwezo, hususan wale watakaohitaji rufaa ya matibabu ya juu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.

“Magonjwa ya moyo yanahitaji uchunguzi wa mapema na matibabu ya haraka. Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma hizi bila kikwazo chochote, hususan kwa wale wasio na uwezo wa kugharamia matibabu,” alisema Makalla.

Aidha, aliwahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akisisitiza kuwa bima hiyo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa gharama nafuu na kwa wakati, huku ikipunguza mzigo wa kifedha kwa familia.

Kwa upande wao, wananchi waliopata huduma hiyo wameipongeza Serikali kwa kuwafikia karibu na makazi yao, wakisema mpango huo umeokoa muda, gharama na umeongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kufanya vipimo vya afya mara kwa mara.

Programu ya vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bure inaendelea kufanyika katika Hospitali ya Seliani, huku matarajio yakiwa ni kuwafikia wananchi wengi zaidi na kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza, hususan magonjwa ya moyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments