📌Ni maelekezo ya Mhe.Rais Samia ya uongezaji thamani madini nchini
📌Waziri Mavunde akagua ujenzi wa kiwanda cha kusindika na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba
📌Kiwanda kuanza uzalishaji Februari,2026
📌Wachimbaji wadogo wapata soko la uhakika wa kuuza malighafi kiwandani
📌Mradi kugharimu Bilioni 37
Tanzania inaendelea kupiga hatua katika Mpango wa Ujenzi wa Viwanda vya Uongezaji Thamani ya Madini, baada ya ujenzi wa kiwanda kipya cha usindikaji na uyeyushaji wa madini ya Nikeli na Shaba kufikia asilimia 85, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayotaka shughuli za uongezaji thamani kufanyika ndani ya nchi kabla ya madini kusafirishwa nje.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 21, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo eneo la Mayamaya, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Mhe. Mavunde amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuwasha mtambo wake wa kwanza wa uzalishaji kufikia Februari 2026, ambapo mtambo huo utakuwa na uwezo wa kuchakata tani 300 za mashapo kwa siku.
Akizungumzia uwekezaji wa kiwanda hicho, Waziri Mavunde amesema jumla ya gharama za ujenzi zitakapokamilika zitafikia shilingi bilioni 37, na hivyo amewataka wachimbaji wadogo nchini kutumia fursa ya soko la uhakika kwa kupeleka malighafi za madini kiwandani hapo.
Amefafanua kuwa dhana ya kujenga viwanda vya uchakataji na uongezaji thamani inalenga kuhakikisha Tanzania inakamilisha mnyororo mzima wa thamani ya madini—kuanzia uchimbaji, uchakataji, hadi uongezaji thamani—ili kusafirisha bidhaa zilizoongezewa thamani badala ya kusafirisha madini ghafi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Joachimu Nyingo, ameipongeza Serikali ya Dkt. Samia kwa kuvutia wawekezaji wa madini katika mkoa wa Dodoma, hatua iliyowezesha kufikiwa kwa viwanda tisa (9) vya uongezaji thamani ya madini hadi sasa.
Naye msimamizi wa kiwanda hicho, Hassan Ngaiza, amesema ujenzi wa kiwanda hicho ukikamilika utaongeza fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii, ikiwemo ajira zaidi ya 300 za kudumu na zisizo za kudumu, upatikanaji wa masoko ya malighafi ya madini na bidhaa nyingine zitakazozalishwa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Metali Tanzania, Thobias Kente, ameushukuru uongozi wa kiwanda cha Zhong Zhou kwa kuhakikisha mradi huo unakwenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati, jambo litakalowanufaisha wachimbaji wadogo wanaohitaji soko la uhakika la madini wanayochimba.







