
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Freeman Mbowe ametangaza kumfikisha Mahakamani aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa na Mbunge wa zamani wa chama hicho ambaye sasa ni kada wa CCM mchungaji Peter Msigwa kutokana na kauli za kumdhalilisha anazozitoa dhidi yake.
Mbowe ametangaza kusudio hilo kupitia barua ya wito aliyomwandikia Mchungaji Msigwa kupitia kwa jopo la mawakili wake watano akiwemo John Mallya, Dickson Matata, Hekima Mwasipu, Simon Mrutu na Jonathan Mndeme.
Katika barua hiyo Mbowe amempa siku tano Msigwa kuchapisha taarifa ya kanusho dhidi ya madai ya kumchafua sambamba na kuomba radhi katika gazeti la kitaifa na gazeti linalosambazwa kikanda, na iwapo hatafanya hivyo basi atamfikisha mahakamani kwa kuwa amemchafua na kushusha heshima yake aliyoijenga kwa miaka mingi ndani ya Chadema na taifa kwa ujumla.
Imeelezwa kuwa Msigwa alidai kuwa Mbowe ameanzisha “Mbowe Foundation,†na anatumia chama cha CHADEMA kwa manufaa yake binafsi. Katika moja ya mikutano yake, Msigwa alinukuliwa akisema, “Mwenyekiti wa CHADEMA amegeuza chama kuwa SACCOS, fedha za chama zinaishia kwenye taasisi binafsi na si kwenye akaunti za chama.â€
Mawakili wa Mbowe wameeleza kuwa matamshi hayo yameathiri sifa ya Mbowe ndani na nje ya Tanzania, hasa kutokana na nafasi zake mbalimbali kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa Naibu Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia vya Afrika (DUA)
Pamoja na hayo Msigwa ametakiwa kumlipa Mbowe faini ya shilingi bilioni tano kama fidia ya madhara aliyomsababishia Mbowe katika kuharibu taswira yake kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Itakumbukwa kuwa Msigwa alijiondoa kuwa mwanachama wa Chadema na kuhamia Chama cha Mapinduzi mwezi Juni,30 mwaka huu ikiwa ni siku kadhaa tu mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kuchagua wenyekiti wa kanda ambapo yeye alitetea nafasi yake lakini alishindwa kwenye king’anyiro hicho.
Tangu wakati huo amekuwa akitoa taarifa zenye ukinzani na tata dhidi ya Mbowe na Chadema akiwa kwenye majukwaa ya kisiasa na katika mitandao ya kijamii.