MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa elimu ya Hifadhi ya Jamii na shughuli zinazotekelezwa na Mfuko huo kwa wajumbe wa baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) jijini Arusha, Februari 10, 2025.

Akitoa wasilisho la utekelezaji wa majukumu ya Mfuko mbele ya wajumbe hao wapatao 100 wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, Afisa Mwandamizi wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Venance Mwaijibe, akiwa amefuatana na Meneja wa Kanda hiyo, Linda Balati, amesema PSSSF imeboresha utoaji wa huduma zake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia lakini pia malengo ya serikali yanayotaka mifumo ya serikali kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma, ambapo kwa sasa mwanachama wa PSSSF anapata huduma zote kupitia mtandao maarufu wa PSSSF Kidijitali.
Mwaijibe alitaja miongoni mwa huduma ambazo mwanachama anazoweza kuzipata kupitia mtandao ni pamoja na taarifa za michango yake, taarifa za uwekezaji, lakini pia namna ya kuwasilisha madai mbalimbali.
“Huduma ya PSSSF Kidijitali inamuwezesha mwanachama kujihudumia mwenyewe kupitia simu janja, kishikwambi (tablet) au kompyuta; huduma hii pia inamuwezesha mwanachama anayekaribia kustaafu, kuweza kuwasilisha madai kupitia mtandao,” amesisitiza.
Aidha, Afisa Mafao Mkuu wa PSSSF Kanda ya Kaskazini, Baraka Kitundu, amesema Mfuko umeanza kutekeleza maagizo ya serikali ya kuanza kulipa mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa na tayari kuanzia Januari mwaka huu wa 2025, pensheni ya kila mwezi imeongezeka kwa asilimia 2.


Amesema, katika maboresho hayo, mstaafu yeyote anayepokea pensheni katika Mfuko wa PSSSF akifariki, Mfuko utatoa kiasi cha Sh 500,000.00 kwa ajili ya maziko (funeral grant), huku mstaafu yoyote akifariki wategemezi wake wanaotambuliwa na sheria ya Mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika, alifafanua Kitundu.
Katika hatua nyingine, jumla ya wanafunzi 11,524 kutoka kaya maskini zilizotambuliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wamenufaika na mkopo wa elimu ya juu kwa asilimia 100 kwa ajili ya kuendelea na masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF, Japhet Boaz, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Vyuo vya Elimu ya Juu (HESLB), iliyofanyika mkoani Arusha.
Boaz amesema, TASAF na HESLB ziliingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na kuweza kuunganisha kanzidata zao ili kuwezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za walengwa kutambulika kirahisi na kuwa wanufaika wa mikopo hiyo kwa asilimia 100.


Amesema wanaishukuru serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kutambua na kuendeleza rasilimali watu kutoka kaya maskini katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha, amesema idadi hiyo ya wanafunzi waliopata mkopo huo ni tangu mwaka 2019/2020 hadi 2024/2025, kitendo ambacho kimepelekea watoto hao kutimiza ndoto zao za kujiendeleza kielimu licha ya kwamba wametoka katika kaya maskini.
Mbali na hilo, amesema kwa kipindi cha miaka 10 TASAF imeweza kuzitambua, kuziandikisha na kuzipatia ruzuku yenye masharti zaidi ya kaya maskini milioni 1.2 zenye zaidi ya wanakaya milioni 5.2 nchini kote katika vijiji na mitaa yote. Amesema miongoni mwa wanakaya tajwa kuna watoto 724,867 wanaosoma shule za msingi, wakati 341,827 wanasoma sekondari (O-level) na 26,308 (A-level).


Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaendeleza juhudi za serikali katika kupunguza umaskini kwa kaya zenye upungufu wa mahitaji ya msingi ili kuziwezesha kaya hizo maskini kuongeza kipato, fursa za kiuchumi na uwezo wa kugharimia mahitaji muhimu na zaidi kujenga rasilimali watu.
