Sunday, November 2, 2025
spot_img
HomeBiasharaSanlam na Allianz zazindua rasmi chapa ya SanlamAllianz Tanzania

Sanlam na Allianz zazindua rasmi chapa ya SanlamAllianz Tanzania

Dar es Salaam, Oktoba, 2025 — Kampuni mbili mashuhuri katika sekta ya bima barani Afrika, Sanlam na Allianz, zimezindua rasmi chapa yao mpya ya SanlamAllianz nchini Tanzania katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huu unafuatia muungano wa makampuni hayo mwaka 2023, uliolenga kuunda kampuni kubwa zaidi barani Afrika inayotoa huduma za kifedha zisizo za benki. Nchini Tanzania, kampuni hizo zimezindua rasmi SanlamAllianz General Insurance Tanzania Ltd na SanlamAllianz Life Insurance Tanzania Ltd, hatua inayoashiria utekelezaji endelevu wa chapa hiyo mpya katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Viongozi wakuu wa kampuni hizo ni Jaideep Goel, Mkurugenzi Mtendaji wa SanlamAllianz General Insurance, na Julius Magabe, Mkurugenzi Mtendaji wa SanlamAllianz Life Insurance.

Kampuni ya SanlamAllianz inalenga kutumia utaalamu wake wa kimataifa wa pan-Afrika kufungua fursa za ukuaji katika masoko ya uchumi yanayokua kwa kasi barani Afrika. Lengo kuu ni kuwezesha vizazi kujiamini kifedha, kuwa na usalama na kustawi, sambamba na kupanua upatikanaji wa huduma za fedha na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kupitia suluhisho bunifu.

Robert Dommisse, Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha SanlamAllianz, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu kwa sekta ya huduma za fedha nchini Tanzania.

“Hii inaonyesha mkakati wetu wa kutumia utaalamu katika masoko yanayokua, kuunda biashara zinazoongoza na kusaidia watu wengi zaidi kupata huduma za fedha. Kupitia ushirikiano huu, tunaunganisha nguvu na uwezo wa kimataifa wa Sanlam na Allianz ili kutoa suluhisho bunifu kwa wateja wetu,” alisema Dommisse.

Kwa upande wake, Jaideep Goel alisema:

“Kipaumbele chetu ni kutoa suluhisho za bima za jumla zenye kuaminika na viwango vya kimataifa. Uzinduzi huu si tu kuhusu chapa mpya, bali ni kuimarisha ahadi yetu ya kusimama na wateja wetu katika kila hatua ya maisha yao.”

Naye Julius Magabe aliongeza kuwa:

“Bima ya maisha ni kuhusu kujenga na kujiamini kwa ajili ya baadaye. Kupitia SanlamAllianz, tunaleta mchanganyiko wa utaalamu wa kimataifa na uelewa wa ndani kusaidia Watanzania kupanga, kulinda na kustawi kifedha. Kipaumbele chetu ni kuzindua bidhaa bunifu zinazochangia usalama wa kifedha wa muda mrefu na ujumuishaji wa kifedha.”

Uzinduzi huu unatarajiwa kuongeza ushindani katika sekta ya bima nchini Tanzania na kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma bunifu za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments