Tuesday, March 3, 2026
spot_img
HomeHabariSerikali yasema miradi ya umeme inasonga mbele kwa ufanisi mkubwa

Serikali yasema miradi ya umeme inasonga mbele kwa ufanisi mkubwa

📌 Akagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Chalinze -Dodoma atoa agizo ukamilike kwa wakati

📌 Asema ni mradi mkubwa wa Sh bilioni 556 unatekelezwa kwa fedha za ndani
📌 MD TANESCO: Msukumo mkubwa unawekwa kusambaza umeme kutoka vyanzo hadi kwa wananchi

📍 Pwani

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa ufanisi, hatua inayoliwezesha taifa kujenga mfumo madhubuti wa upatikanaji wa nishati ya uhakika.

Ametoa kauli hiyo Novemba 27, 2025, alipofanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambapo alisisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Waziri Ndejembi ameeleza kuwa mradi huo mkubwa unatekelezwa kwa fedha za ndani, na utakapoakamilika utakuwa umegharimu takribani shilingi bilioni 556.

“Niwaagize TANESCO kuendelea kumsimamia Mkandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kulingana na ratiba. Hatutaki kufika mwisho wa utekelezaji na kukuta mradi umekabidhiwa bila kukamilika,” amesema.

Aidha, amesema TANESCO imeelekezwa kukutana na Mkandarasi ili kuandaa mpango kazi mpya utakaoweka wazi hatua za ufuatiliaji hadi ukamilishaji wa mradi huo muhimu.

Waziri Ndejembi ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kutoa msukumo mkubwa kuhakikisha wananchi kote nchini wanapata umeme wa uhakika na kwa ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Tanzania ina umeme wa kutosha kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali, na kwamba juhudi zinazofanyika sasa ni kuupeleka umeme huo kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda kwa wananchi na wawekezaji.

Ameeleza kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa vituo vikubwa vya kupokea na kupoza umeme katika Dodoma na Chalinze, ambavyo vitakuwa kitovu cha kusafirisha umeme kutoka Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) na chanzo kingine chochote kuelekea maeneo ya nchi.

“Kituo cha kupokea umeme cha Dodoma ni njia muhimu inayopokea umeme kutoka maeneo mbalimbali, na pia ndicho kinachotuunganisha na wenzetu nchini Kenya,” amesema Twange.

Ameongeza kuwa hatua hizo ni msingi katika kujenga mfumo imara wa umeme utakaoendana na mahitaji ya sasa na ya vizazi vijavyo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments