Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kimesema kuwa elimu ya akiolojia inayotolewa na Makumbusho ya Ngorongoro–Lengai UNESCO Global Geopark, iliyopo Karatu mkoani Arusha, imeibuka kuwa eneo la kipekee la kujifunza umahiri wa kisayansi kuhusu historia ya binadamu na masalia ya kale.
Jiopaki ya Ngorongoro–Lengai ni ya kipekee Kusini mwa Jangwa la Sahara na inabeba sifa ya kuwa na volkano hai, ikiwa ni ya pili barani Afrika baada ya ile ya M’Goun nchini Morocco.
Mhadhiri wa SUZA, Dk. Abdallah Mkumbukwa, akizungumza mwishoni mwa wiki baada ya kuongoza wanafunzi wa elimu ya juu katika mafunzo ya vitendo, alisema makumbusho hayo kwa sasa ni “kisima cha elimu” kinachotoa umahiri mpana katika fani za akiolojia, miamba, jiolojia na utamaduni ndani ya Bara la Afrika.


“Kuja kwetu hapa kujifunza kwa vitendo kuhusu akiolojia ni darasa kubwa kwa wanafunzi wa SUZA,” alisema. “Imewawezesha kuunganisha nadharia wanazofundishwa darasani na uhalisia wa kisayansi na kimazingira. Tumepata maarifa mapya kuhusu muonekano wa dunia katika enzi za kale, maumbile asilia ya Bonde la Ufa, na hata kuona mwamba wenye umri wa miaka milioni tatu katika hifadhi hii.”
Dk. Mkumbukwa aliongeza kuwa wanafunzi pia wamejifunza kuhusu tamaduni za makabila mbalimbali yanayopatikana eneo hilo, yakiwemo Wahadzabe, Wairaqw, Wadatoga na Wamasai—urithi unaoonekana na kuelezwa kwa ustadi ndani ya makumbusho hayo.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro–Lengai, Afisa Uhifadhi Mkuu Dk. Agness Gidna, alisema tangu yalipofunguliwa mwezi Oktoba mwaka huu, makumbusho hayo yameendelea kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema wageni hao, pamoja na kutalii, wanajifunza masuala ya akiolojia na urithi wa kiutamaduni kupitia maonyesho na taarifa mbalimbali zilizopo.
Dk. Gidna alieleza kuwa ziara ya wanafunzi wa SUZA imewachochea kujua zaidi kuhusu historia ya sayansi, mazingira, jiografia, jiolojia na masuala mapana ya utamaduni—na kuongeza kuwa makumbusho hayo yanatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha elimu ya kihistoria na kisayansi kwa vizazi vijavyo.





