Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimekanusha taarifa zilizosambaa kwamba huduma za usafiri wa mabasi zitasitishwa kesho, Oktoba 29, 2025, kupisha Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha ITV, Naibu Katibu wa TABOA, Issa Nkya, amesema huduma za usafiri zitaendelea kama kawaida kwa saa 24, na abiria wanaruhusiwa kusafiri muda wowote kulingana na mahitaji yao.
“Huduma zinaendelea kama kawaida. Tumejiandaa kuhudumia abiria, na wengi wamekuwa wakipenda kusafiri kuanzia saa tisa alasiri,” amesema Nkya.
Ameongeza kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha abiria wote wanafika katika maeneo yao salama, huku akiwataka wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi zinazosambaa mitandaoni.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti awali kwamba huduma za mabasi zingesitishwa kupisha uchaguzi, taarifa ambazo TABOA imezitaja kuwa hazina ukweli wowote.




