Tabora United yajichimbia ikiwaza pointi 9

KIKOSI cha Tabora United kimeondoka Tabora Mjini na kwenda kuweka kambi sehemu ambayo haijatajwa kwa ajili ya kujiwinda kuikabili Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Septemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, imeelezwa.

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala, amesema hawataki timu yao ijulikane ilipoweka kambi kwa sababu wanahitaji kujiimarisha na kuwa imara ili kupata ushindi katika mchezo huo ujao.

Mwagala alisema lengo ni kuwapa benchi la ufundi muda mzuri wa kuandaa kikosi, lakini kuleta utulivu kwa wachezaji wao, kabla ya mechi hiyo dhidi ya Kagera Sugar na nyingine mbili zinazofuata ambazo watacheza nyumbani.

“Tumeamua timu iendelee kukaa kambini, lakini tumeondoka Tabora, tumeweka kambi sehemu ambayo hatusemi, lakini ni nje ya hapa.

Hatutaki kambi yetu ijulikane kwa sababu kocha anahitaji muda zaidi na wachezaji wetu wanahitaji utulivu kwa sababu tunahitaji pointi tisa katika mechi zote tatu tutakazocheza nyumbani, tukianzia na Kagera Sugar,” alisema Mwagala.

Aliongeza wanaamini kikosi chao kitaimarisha na kupata pointi tisa kutoka kwenye michezo hiyo mitatu mfululizo ambayo watacheza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Fountain Gate.

“Tuna mechi dhidi ya Kagera Sugar, Septemba 11, lakini baada ya hapo tutakuwa na michezo mingine ya nyumbani tukiwaalika Prisons na baadaye Fountain Gate, baada ya hapo tutatoka kwenda Mbeya kucheza dhidi ya KenGold Septemba 28, mwaka huu, sasa kabla hatujaondoka nyumbani mkakati wetu ni kuzipata pointi zote tisa tutakazocheza hapa,” Mwagala alisema.

Tabora United imecheza michezo miwili mpaka sasa, ikiwa na pointi tatu, ikichapwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Simba, kabla ya kuifunga Namungo mabao 2-1 na kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba yenye pointi sita ndio kinara wa ligi hiyo ikifuatiwa na Singida Black Stars ambayo pia imeshinda mechi zake mbili ilizocheza huku mabingwa watetezi, Yanga wana pointi tatu wakishuka dimbani mara moja na kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Chanzo: Nipashe/Ippmedia.com

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *