Serikali ya Tanzania na Marekani zimefikia hatua ya mwisho ya majadiliano, ili kutia saini na kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Gesi Asilia ya Kimiminika (LNG) wenye thamani ya Dola bilioni 42 (zaidi ya Sh 102.9).
Hatua hiyo ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na Kaimu Balozi wa Marekani, Andrew Lentz Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, kwa mazungumzo kuhusu mradi huo na mingine miwili ya Tembo Nickel ( na Mahenge Graphite.
Katika mazungumzo ya wawili hao, Balozi Lentz amesema Marekani imejipanga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama, akibainisha msimamo wa Taifa hilo ni kujenga ushirikiano kwa ustawi wa pamoja badala ya utegemezi.
Amesema mazingira ya sasa ya Tanzania ni thabiti kwa uwekezaji na yanafungua fursa zaidi kwa sekta binafsi ya Marekani.

Kwa upande wake, Rais Samia ameiambia Marekani kuwa, Tanzania isiyofungamana na upande wowote, iko tayari kushirikiana na mataifa yote yanayoheshimu mamlaka na masilahi yake.
Pia, amesema zaidi ya kampuni 400 za Marekani tayari zinafanya kazi nchini, ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.




