Timu ya taifa ya wanawake ya Futsal imeanza kwa kusuasua kwenye Kombe la Dunia baada ya kukubali kipigo cha mabao 10–0 kutoka kwa Ureno katika mchezo wa Kundi C uliochezwa Manila, Ufilipino. Ureno walitawala mchezo kwa dakika zote, wakifunga mabao matano kila kipindi huku Tanzania ikionekana kufanya makosa mengi.
Kocha Mkuu wa Tanzania, Curtis Reid, alisema kikosi chake bado kinajifunza kutokana na uzoefu mdogo wa mchezo huo nchini.
“Wenzetu wamecheza Futsal kwa miaka mingi na ndiyo maana tumeona utofauti mkubwa wa mbinu. Sisi tupo kwenye kujifunza na naamini tutaimarika kadri muda unavyokwenda,” alisema.
Matokeo hayo yanaifanya Tanzania kuwa timu ya kwanza kufungwa mabao mengi tangu kuanza kwa michuano Novemba 21. Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Japan iliifunga New Zealand mabao 6–0.
Tanzania inatarajiwa kurudi uwanjani keshokutwa kuivaa New Zealand kabla ya kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Japan Novemba 29. Ili kusonga mbele, ni lazima ipate matokeo mazuri kwenye mechi mbili zijazo.
Futsal ni mchezo mpya nchini Tanzania na kwa mara ya kwanza timu ilishiriki mashindano ya Afrika mwezi Mei Morocco, ambako ilitwaa nafasi ya pili na kufuzu kwa Kombe la Dunia.




