Monday, December 8, 2025
spot_img
HomeBiasharaUuzaji wa samaki nje ya nchi wapaa hadi bilioni 755

Uuzaji wa samaki nje ya nchi wapaa hadi bilioni 755

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema kuwa uuzaji wa samaki nje ya nchi umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka tani 42,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 509.9 hadi kufikia tani 59,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 755.

Akihitimisha Maadhimisho ya Siku ya Mvuvi Duniani yaliyofanyika katika fukwe za Kawe Beach jijini Dar es Salaam kwa siku mbili mfululizo (20–21 Novemba 2025), Meena pia amesema sekta ya uvuvi imeendelea kukua kwa kasi, hatua inayoonekana pia kwenye ongezeko la idadi ya wavuvi kutoka 198,475 mwaka 2023 hadi 201,661 mwaka 2024, pamoja na kuongezeka kwa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi kutoka 21 hadi 64 katika kipindi hicho.

Meena amesema dhana ya Uchumi wa Buluu inaendelea kupewa kipaumbele nchini kutokana na nafasi yake muhimu katika kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni sita, sawa na asilimia 10 ya watu wote nchini.

“Tanzania imebarikiwa rasilimali nyingi za maji—bahari, mito, mabwawa, maziwa na maeneo oevu. Serikali itaendelea kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, ufugaji wa samaki kwa vizimba na mabwawa, na kuandaa mikakati ya usimamizi wa rasilimali hizi ili kuongeza uzalishaji, kupunguza uharibifu wa mazingira na kuzuia uvamizi wa fukwe,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili umeongezeka kutoka tani 479,976 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 hadi tani 522,788 zenye thamani ya shilingi trilioni 4.3 mwaka 2024, ikiwa ni matokeo ya jitihada endelevu za Serikali katika usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo, Emelda Teikwa, amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau imefanya maadhimisho haya kwa wakati mmoja katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uelewa wa wavuvi kuhusu uhifadhi wa mazingira, usafi wa fukwe na uvuvi endelevu.

Amesema utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka huu umewezeshwa na ushirikiano kati ya wizara na wadau mbalimbali wanaosaidia kufanikisha malengo ya sekta, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kulinda rasilimali za maji.

Katika kutoa salamu za wavuvi, Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) Kawe Beach, Mudu Mohamed, ameomba Serikali kudhibiti uvamizi wa fukwe unaoendelea kukithiri katika maeneo ya Kawe, Kunduchi, Msasani, Mbweni na Ununio, akisema unahatarisha mazingira, shughuli za uvuvi na fursa za kibiashara kwa vijana na kina mama.

Ameiomba Serikali kuongeza boti kwa BMU ili kuimarisha doria na kulinda rasilimali za baharini, sambamba na kuimarisha ulinzi wa maeneo ya fukwe.

Katika siku ya kwanza ya maadhimisho, shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja na kampeni za usafi wa mazingira na fukwe, midahalo ya utoaji elimu kwa wavuvi, pamoja na uhamasishaji wa ulaji wa samaki kwa manufaa ya afya.

Pia, Katibu Mkuu Meena alizindua Mpango wa Kitaifa wa Usimamizi wa Samaki Aina ya Jodari, pamoja na mpango wa uhifadhi wa samaki aina ya papa na taa, huku pia akitembelea mabanda ya maonesho kuona bidhaa mbalimbali za mazao ya uvuvi.

Maadhimisho ya mwaka huu yalibebwa na kaulimbiu isemayo:
“Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji Endelevu: Msingi Imara wa Uchumi wa Buluu.”

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments