Tuesday, December 9, 2025
spot_img
HomeHabariWaandishi 100 wajengewa uwezo kuandika habari za amani

Waandishi 100 wajengewa uwezo kuandika habari za amani

Na Neema Emmanuel

Zaidi ya waandishi wa habari 100 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wamejengewa uwezo kupitia mafunzo maalum ya uandishi wa habari za amani, lengo likiwa kuimarisha weledi na kupunguza upotoshaji katika jamii.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko, amesema mafunzo hayo ni awamu ya kwanza, na tayari kunaratibiwa awamu nyingine zitakazowafikia jumla ya waandishi 400 nchini.

Amesema mafunzo hayo yanawapa waandishi uwezo wa kuandika habari zinazohamasisha amani, kupunguza taarifa zenye viashiria vya uchochezi, uchochezi wa migogoro, lugha za chuki na upotoshaji.

Aidha, yanawawezesha kuchambua taarifa zenye dalili za kuathiri umoja wa kitaifa na badala yake kuandika habari zinazojenga mshikamano na uzalendo.

Kwa mujibu wa Soko, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha vyombo vya habari nchini vinaendelea kuwa nguzo muhimu ya kudumisha amani, hasa wakati huu ambao taarifa potofu zinazosambaa mitandaoni zimeongezeka kwa kasi.

Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP David Misime, ametoa rai kwa waandishi na vyombo vya habari kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi, zilizohakikiwa na zisizo na mwelekeo wa uchochezi, ili kulinda amani, umoja na utulivu wa taifa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments