Wananchi wa Mkoa wa Arusha wamejumuika kushiriki katika kampeni ya uhamasishaji kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, ambapo walipata elimu ya moja kwa moja kupitia maonyesho na mafunzo yaliyotolewa na wataalamu. Washiriki walifundishwa faida za kupika kwa njia salama, bora na endelevu kwa afya na mazingira.

Kampeni hiyo ni mwendelezo wa mpango ulioanzishwa mwezi Juni mwaka huu kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la UKAid na programu ya MECS.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa 2024–2034, unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya kaya nchini zinatumia nishati safi ya kupikia.
Kupitia kampeni hizi, Serikali na wadau wanatarajia kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kuachana na matumizi ya nishati zenye madhara kiafya na kimazingira, na badala yake kukumbatia mbinu za kisasa zinazochangia ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.








