Saturday, February 7, 2026
spot_img
HomeBiasharaWatu Simu Tanzania yawafikia wateja milion 1 wa simu janja

Watu Simu Tanzania yawafikia wateja milion 1 wa simu janja

📌Milioni Moja – Tunasonga Mbele Kidigitali

Kampuni ya Watu Tanzania imefikia hatua muhimu ya kihistoria baada ya kuwezesha Watanzania milioni moja kumiliki simu janja kupitia huduma yake ya Watu Simu, mpango wa kidigitali unaolenga kupanua upatikanaji wa nyenzo za kidigitali kwa kutumia mfumo rafiki wa malipo ya awamu (pay-as-you-go).

Watu ni kampuni ya ufadhili wa mali iliyopewa leseni na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayotoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mali zinazozalisha kipato, ikiwemo pikipiki kwa waendesha bodaboda pamoja na simu janja zinazowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali. Kadri kampuni inavyoelekea kutimiza miaka mitano ya shughuli zake za kibiashara nchini Tanzania, mafanikio haya yanaonesha ukubwa na kasi ya ukuaji wa Watu Simu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kidigitali nchini.

Katika mazingira ya sasa ambapo simu janja zimekuwa lango kuu la malipo, huduma, mawasiliano na uzalishaji wa kipato, kufadhili simu janja milioni moja kunawakilisha upanuzi mkubwa wa ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa kidigitali. Kupitia hatua hii, Watu Simu siyo tu kwamba inaongeza upatikanaji wa nyenzo hizi muhimu, bali pia inaunga mkono ajenda ya Serikali katika mageuzi ya kidigitali na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi zinazotegemea teknolojia.

Kwa kiwango hiki cha upatikanaji na matumizi ya huduma za kidigitali, umiliki wa simu janja unaendelea kuwa kigezo cha msingi kinachoamua nani anaweza kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaoendeshwa na teknolojia.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Meneja Mkazi wa Watu Tanzania, Rumisho Shikonyi, amesema kuwa simu janja si anasa tena kwa walaji bali ni nyenzo muhimu katika shughuli za kila siku za kiuchumi.

“Simu janja si anasa tena. Ni nyenzo muhimu katika ushiriki wa shughuli za kiuchumi za kila siku. Kufikia mafanikio ya kuwezesha Watanzania milioni moja kumiliki simu janja kupitia Watu Simu ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa muda mrefu, unaoonesha nafasi yetu kama mfadhili katika kuwezesha upatikanaji wa nyenzo za kidigitali zinazosaidia uzalishaji, ajira na ushiriki mpana wa kiuchumi,” amesema Shikonyi.

Huduma ya Watu Simu inaongeza thamani katika biashara kuu ya kampuni ya kufadhili pikipiki, kwa kutambua kuwa sekta ya usafirishaji na muunganiko wa kidigitali vinafanya kazi kwa pamoja katika kusaidia uzalishaji wa kipato. Wakati pikipiki zinawezesha usafiri na upatikanaji wa ajira, simu janja huwezesha uratibu wa kazi, malipo, mawasiliano pamoja na ufikiaji wa masoko na majukwaa mapana ya biashara za kidigitali.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), matumizi ya simu janja yanaendelea kuongezeka nchini, hali inayoonesha umuhimu wa umiliki wa simu hizo pamoja na uwezeshaji wa kifedha unaowasaidia wananchi kushiriki kwa tija katika uchumi wa kidigitali. Katika muktadha huo, ukubwa wa huduma ya Watu Simu unaakisi mchango muhimu wa ufadhili wa nyenzo hizi katika kujenga mazingira wezeshi ya ushiriki wa kidigitali kwa wote.

Hadi sasa, Watu Simu inafanya kazi katika mikoa yote 26 ya Tanzania, ikihakikisha upatikanaji wa simu janja kote nchini na kuwahudumia watu binafsi, familia pamoja na biashara ndogo ndogo katika maeneo ya mijini na vijijini.

Shughuli za uendeshaji wa Watu zinazingatia mifumo wazi ya marejesho ya mikopo, matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na uwepo wa timu imara za wafanyakazi wa ndani nchini kote. Mikakati hii imeiwezesha kampuni kukua kwa uwajibikaji huku ikizingatia sheria na kanuni za uendeshaji, kulinda haki za wateja na kujenga uaminifu wa muda mrefu.

Kadri Tanzania inavyoendelea na safari yake ya mageuzi ya kidigitali, Watu inaendelea kujikita katika ufadhili wenye uwajibikaji kwa kuwezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika uchumi wa kidigitali na kusaidia shughuli endelevu za kiuchumi nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments