Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje amewataka wananchi wasikubali kushikiwa akili katika kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Ameeleza haki hiyo ni ya kikatiba na inapaswa kila mmoja ahakikishe anaitimiza bila kukubali mkumbo wa vyama vya siasa vinavyowazuia kulitekeleza hilo.
Wenje ameyasema hayo leo, Jumanne Oktoba 28, 2025 alipozungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza.
Amesema kupiga kura ni haki ya mwananchi mmoja mmoja na asitokee mtu anayeshawishiwa na chama cha siasa kuacha kuitimiza haki hiyo.
“Nchi hii ina utaratibu, suala la kwenda kupiga kura sio suala la vyama vya siasa ni suala la Mtanzania mmoja mmoja, hii ni haki yako binafsi.
“Wana CHADEMA suala la haki yako ya kupiga kura, usikubali idhibitiwe na chama cha siasa, nenda kapige kura usikubali akili yako kushikiwa na mtu,” amesema.




