Maofisa wa usafirishaji bodaboda na wafanyabiashara machinga wa mkoa wa Dar es Salaam wametangaza kuwa hawatafungua shughuli zao Desemba 9, 2025 kufuatia taarifa za uwepo wa maandamano yanayodaiwa kuratibiwa kinyume cha utaratibu wa kisheria.
Wakizungumza leo Jumapili, Novemba 29, 2025 katika kikao chao kilichowakutanisha na wakuu wa wilaya mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, wamesema uamuzi wao unatokana na nia ya kudumisha amani na kuepuka kuchanganywa katika vurugu zisizokuwa rasmi.
Wamesema wamewaonya wenzao wanaojishughulisha na biashara na usafirishaji kuwa ni muhimu kubaki majumbani siku hiyo, na kwamba yeyote atakayekiuka na kujiingiza katika maandamano yatakayojitokeza, atawajibika binafsi.
“Hatufungua maeneo yetu ya biashara, maana wanaweza kusema machinga walikuwa wanaandamana,” walisema. “Tutazungumza na wenzetu kupitia kusanyiko hili. Tutafunga biashara ili yule atakayekwenda Kariakoo kwa kisingizio cha machinga atakumbana na mkono wa dola. Sisi tunataka amani na utulivu.”
Wakuu wa wilaya waliohudhuria kikao hicho walisisitiza umuhimu wa jumuiya hizo kushirikiana na Serikali katika kudumisha utulivu na kutii taratibu za kisheria wakati wote.




