Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ni nchi huru haitakubali kupangiwa namna ya kufanya mambo yake na mataifa mengine kwa kisingizio cha misaada au kitu kingine chochote kile, badala yake itaamua mambo yake kadiri ya mahitaji ya watu wake.
Akiongea na wazee wa Dar es Salaam, Desemba 02, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere Rais Samia alisema baadhi ya mataifa wamekuwa wakiunga mkono madai yasiyokuwa na msingi ya baadahi ya vyama vya siasa kwa malengo ya kuivuruga nchi.
Alisema baadhi vya vyama vya siasa vilijitoa vyenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu, kwa kuogopa kushindwa na sasa wanatafuta visingizio kwa kusaidiwa na kufadhiliwa na watu wa nje.
“Katika ile aibu ya kuepuka kushindwa uchaguzi wanaweka visingizio. Visingizio vyote hivi vinaungwa mkono na nje (mataifa ya nje) hawana hata aibu, nje huko wanakaa wanasema Tanzania ifanye moja, ifanye mbili, ifanye tatu, halafu ndiyo itakuwa hivi, who are you?,” alihoji Rais Samia.
“Niwaulize ndugu zangu, kwao hayatokei? Tumenyanyua sauti kusema ya kwao? Wanadhania bado wao ni wakoloni kwetu? Kitu gani? ni fedha chache wanzotugawia, na fedha yenyewe sasa haipo, tunafanya biashara ili wao wapate na sisi tupate ndipo tunaposimamia.”
Alisema Tanzania ni kama mwanake mzuri ambaye anapiganiwa na wanaume wawili na kwamba siasa ya kutofungamana na upande wowote ambayo haibagua mtu wa kushirikiana naye ndiyo inayowasumbua kwa kuwa kila mtu anavuta upande wake.
Aliwataka watanzania kutambua kuwa nchi ina utajiri mwingi wa rasilimali na hizo zimekuwa chanzo cha chokochoko za mataifa ya nje na hivyo kuwataka kushikamana, kuwa imara na kulilinda taifa lao.




