Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji Oktoba 6, 2026 amefanya ziara katika maeneo yaliyoathiriwa na moto katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na kubaini miongoni mwa makundi ya watu wanaoanzisha mioto katika hifadhi hiyo.
Kwa kutumia helikopta na teknolojia ya ndege nyuki Waziri Kijaji akiambatana na Maafisa wa Jeshi la Uhifadhi, vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Kikosi cha Jeshi la Zimamoto wamebaini uwepo wa majangiri wanaofanya shughuli haramu katika hifadhi zikiwemo uwindaji na ukataji miti kwaajili ya kutengeneza nguzo, ikishuhudiwa maeneo kadhaa ambayo majangiri hao wameweka kambi zao ambapo wamewasha mioto kwaajili ya shughuli zao haramu.
Waziri Kijaji amesema Serikali itahakikisha watu hao wenye nia ovu na Taifa wanatiwa nguvuni na hatua Kali zitachukuliwa dhidi yao, aidha amevipongeza vikosi vya Jeshi la Uhifadhi pamoja na vikosi vya Ulinzi na Usalama na vile vya Jeshi la Zima Moto kwa jitihada kubwa zilizopelekea hadi sasa moto huo kuwa umedhibitiwa Kwa kiasi kikubwa.
Vilevile Waziri Kijaji amewashukuru wadau katika sekta ya uhifadhi na utalii kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika kukabiliana na moto huo kwa kuwezesha huduma mbalimbali ikiwemo nguuvukazi katika kuzima moto, huduma za afya na vyakula kwa vikosi vilivyopo uwandani kuzima moto.
Dkt. Kijaji ametoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo jirani na Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kushirikiana na Serikali kwa kufichua mipango ya vitendo viovu na wote wanaohusika katika shughuli za ujangiri ili hifadhi hiyo iendelee kuwa salama kwa manufaa ya watanzania wote.




