Watoto nchini wanatarajiwa kunufaika na uboreshaji wa ufundishaji wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), kupitia ushirikiano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Shirika la Room to Read, unaolenga kuimarisha vifaa vya kujifunzia, uwezo wa walimu na upatikanaji wa elimu bora kwa usawa.
Ushirikiano huo unalenga kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa KKK, ambao unasisitiza kuhakikisha hakuna mtoto anayefika Darasa la Tatu bila kuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu.
Hayo yameelezwa Novemba 4, 2026, wakati TET na Room to Read Tanzania zinasaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika Ofisi za TET, Dodoma. Makubaliano hayo yanaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa TET amesema makubaliano hayo yana maeneo makuu matatu, ambayo ni kuandaa, kupitia na kuboresha vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyoendana na mitaala ya taifa; kuimarisha umahiri wa walimu kupitia mafunzo ya awali na endelevu; na kuwezesha upatikanaji wa elimu bora bila ubaguzi.
Amesema ushirikiano huo utatekelezwa kupitia programu za KKK, usawa wa kijinsia na ushirikiano wa kitaalamu kati ya taasisi hizo mbili.
Katika eneo la vifaa vya kujifunzia, TET itashirikiana na Room to Read kuandaa na kupitia vitabu vya hadithi, nyenzo za kujisomea, moduli za stadi za maisha na elimu ya fedha, pamoja na miswada ya maudhui ya video za kielimu.


TET pia itahakikisha vifaa hivyo vinakidhi viwango vya ubora na kuidhinishwa kwa matumizi katika mfumo wa elimu nchini. Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nyenzo zinazokidhi mahitaji ya wanafunzi na kuendana na mtaala wa taifa.
Kwa upande wa walimu, makubaliano hayo yanajumuisha kuimarisha uwezo wao kupitia mafunzo ya awali na mafunzo endelevu ya kitaaluma. Aidha, moduli ya stadi za maisha inatarajiwa kuandaliwa kwa ajili ya programu ya mafunzo endelevu ya walimu ya MEWAKA na kuwekwa katika mfumo wa kidijitali wa TET (LMS).
Katika utekelezaji wake, TET itatoa vibali kwa maeneo yatakayochaguliwa kufanyiwa majaribio ya programu, kushiriki tathmini ya matokeo na kusimamia ufuatiliaji. Taasisi hiyo pia itashirikiana katika kampeni ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu chake, pamoja na kuratibu uchapishaji na usambazaji wa vitabu vitakavyoidhinishwa.
Eneo jingine ni usawa wa kijinsia na elimu jumuishi, ambapo ushirikiano huo unalenga kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapata fursa sawa za elimu bora bila kubaguliwa.
Programu za stadi za maisha zitajikita katika kuwajengea vijana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujenga mahusiano yenye afya, kufikiri kwa kina, kukabiliana na changamoto na kuendeleza uongozi. Stadi hizo zinatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha na kushiriki kikamilifu katika jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Room to Read Tanzania, Joan Ndaambuyo Minja, amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali kupitia TET tangu mwaka 2012 katika kuboresha uwezo wa watoto kusoma na kuandika.
Amesema ushirikiano huo umehusisha uandaaji wa vitabu vya hadithi na vifaa vya kujifunzia, pamoja na moduli za stadi za maisha kwa vijana, ambazo hupitiwa na kuidhinishwa na TET kabla ya kutumika.
Ameeleza kuwa mwaka 2021, Room to Read ilishiriki katika warsha za kuboresha ufundishaji wa kusoma katika elimu ya awali na msingi. Ushirikiano huo pia ulichangia mchakato wa kuboresha mtaala wa kitaifa wa ufundishaji wa kusoma na kuandika kwa wanafunzi wa Darasa la Kwanza na la Pili.
Amesema shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano katika upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia, kujenga uwezo wa walimu, kuongeza vitabu shuleni na kuimarisha maktaba za shule na jamii.
Ushirikiano huo unaendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa KKK uliozinduliwa Januari 2026.
Kwa mujibu wa TET, makubaliano hayo yanatarajiwa kuchangia utekelezaji wa programu za elimu kwa kuimarisha ubora wa vifaa vya kujifunzia, uwezo wa walimu na mazingira yanayowezesha watoto wote kupata elimu yenye usawa.





