✍🏿…….Uchumi wa buluu unahusisha uvuvi, usafirishaji, utalii, gesi, petrol na umwagiliaji.
Utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu umetajwa kuwa lango kuu la uchumi kutokana na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye sekta hiyo.
Sekta ya uchumi wa buluu inahusisha mambo sita ambayo ni uvuvi, usafirishaji, utalii, gesi, petrol na umwagiliaji.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uchumi wa Buluu na Uratibu Ofisi ya Makamu wa Rais, Magdalena Ngotolainyo, wakati akizungumzia uchumi wa buluu.
Alisema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa si kwa ardhi yenye rutuba pekee, wala si kwa madini, wanyamapori na vivutio vya utalii pekee, bali pia kwa utajiri mkubwa uliomo ndani ya maji yake. Bahari, maziwa, mito, mabwawa, maeneo oevu, maji chini ya ardhi na ukanda mpana wa pwani ni hazina ya kipekee ambayo, ikitumika kwa maarifa na uendelevu, inaweza kuwa injini mpya ya mageuzi ya kiuchumi na ustawi wa wananchi. Hii ndiyo nguvu ya Uchumi wa Buluu.

Alisema uchumi wa buluu unahusisha matumizi endelevu ya rasilimali zinazopatikana katika bahari, maziwa, mito, mabonde ya maji, maeneo oevu na maji yaliyo chini ya ardhi kwa ajili ya kukuza uchumi, kuboresha maisha ya jamii na kulinda mazingira. Kwa Tanzania, dhana hii si nadharia ya mbali.
“Ni uhalisia unaoonekana katika kila pembe ya nchi: kuanzia Bahari ya Hindi hadi Ziwa Victoria, kutoka Ziwa Tanganyika hadi Ziwa Nyasa, na kutoka mito mikubwa hadi ukanda wa pwani wenye fursa zisizohesabika,” alisema.
Aidha, alisema kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024, Tanzania ina rasilimali kubwa za maji zinazoweza kuwa msingi imara wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Alisema Tanzania ina takribani kilomita za mraba 61,500 za maeneo ya maji baridi yanayofaa kwa matumizi mbalimbali, yanayokadiriwa kuwa na mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka. Aidha, Tanzania ina kilomita za mraba 64,000 za maji ya kitaifa katika bahari na kilomita za mraba 223,000 za Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Bahari.
“ Haya si maeneo ya kijiografia tu; ni maeneo ya fursa, ajira, uwekezaji na maendeleo,” alisema.
Aidha, alisema ukanda wa pwani wa Tanzania wenye urefu wa kilomita 1,424 ni lango muhimu la uchumi wa taifa. Pwani hii inawezesha shughuli za uvuvi, usafirishaji wa baharini, utalii wa fukwe, ukuzaji wa viumbe maji, uhifadhi wa mazingira na biashara ya kimataifa.
Alisema Bandari rasmi 86 na zisizo rasmi 885 zilizopo nchini zinaonesha namna Tanzania ilivyo na nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na nchi jirani zisizo na bahari.




